Ticker

6/recent/ticker-posts

KRISTO ALIAGIZA TUKUMBUKE ‘SIKU YA PASAKA’ AU ‘MEZA YA BWANA’? JE, ‘PASAKA’ NI ‘SIKU’? ‘PASAKA’ NI SAWA NA ‘EASTER’?





KRISTO ALIAGIZA TUKUMBUKE ‘SIKU YA PASAKA’ AU ‘MEZA YA BWANA’? JE, ‘PASAKA’ NI ‘SIKU’? ‘PASAKA’ NI SAWA NA ‘EASTER’?

UTANGULIZI

Ni ukweli usiopingika kwamba kufa na kufufuka kwa Kristo ndilo tumaini letu. Kama Kristo hangekufa na kufufuka (kushinda kifo) imani yetu ingekuwa ni bure kabisa. 1 Kor 15:14,17-20 tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

Kumbuka siku ya sabato ilianzishwa wakati wa uumbaji kabla ya anguko (dhambi). Adamu alipoanguka alituuza kwa shetani hivyo tukahukumiwa na kupotea milele. Mungu akamtuma Adamu wa mwisho ili ajaribiwe kama Adamu wa kwanza na kutununua (kutukomboa) kwa vile shetani alikuwa anatumiliki kihalali kutokana na kosa la Adamu wa kwanza. 1 Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.” Adamu wa kwanza alikuwa ni nafsi iliyo hai (living being) na Adamu wa mwisho (Yesu Kristo) akawa ni roho inayohuisha (life-giving Spirit).

Kwa vile kufufuka kwa Yesu ndiko kumerudisha thamani ya mwanadamu na uhusiano wake na Mungu, Kanisa la kwanza walianza kuabudu siku ya kwanza ya juma (siku aliyofufuka Bwana Yesu). Mdo 20:7 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.” 1 Kor 16:2 “Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.”

Bwana Yesu akiwa duniani kimwili aliadhimisha Pasaka hadi Yeye mwenyewe alipofanyika Pasaka kwa ajili yetu. Hata hivyo Pasaka haikusherehekewa kama ilivyo leo bali kulikuwa na mwongozo maalum. Yohana 11:55 “Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase.”

UHUSIANO WA “PASAKA”, “MEZA YA BWANA” NA “KRISTO”

1. Pasaka ilianzishwa na Mungu kwa ajili ya taifa la Israeli wakati meza ya Bwana ilianzishwa na Kristo kwa ajili ya Wakristo.

Israeli waliagizwa kuikumbuka SIKU HII lakini Kristo aliagiza akumbukwe YEYE MWENYEWE kwa njia ya MEZA YA BWANA

Pasaka ilianzishwa kwa ajili ya Waisraeli. Kut 12:12-14 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.”

Meza ya Bwana ilianzishwa na Kristo kwa ajili ya Wakristo. Lk 22:19 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

2. Pasaka na Meza ya Bwana vyote vilianzishwa na Mungu ‘usiku’ kabla ya tukio la ukombozi.

3. Pasaka na Meza ya Bwana vyote vilihusisha mwanakondoo.

Tulinganishe mwanakondoo (mnyama) na Mwanakondoo (Kristo)

Pasaka ya Israeli – mwanakondoo (mnyama) Kut 12:3 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja.”

Pasaka ya Wakristo – Mwanakondoo (Kristo) 1 Kor 5:7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.”

(i).  Mwanakondoo alitakiwa kuwa mume aliyekomaa (awe amekomaa anayeweza kujisimamia bila kuwa tegemezi kwa mama yake)

Mwanakondoo alitakiwa kuwa mume wa mwaka 1. Kut 12:5 “Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.”

Kristo ana sifa hizi za mwanakondoo.

Katika Agano la Kale watu waliingia katika utumishi wa hema ya kukutania kati ya umri wa miaka 30 hadi 50.

Hes 4: 2,3 “Katika wana wa Lawi uitenge hesabu ya wana wa Kohathi, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao, tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi hata umri wa miaka hamsini, wote waingiao katika utumishi huo, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.”

Kristo alianza rasmi huduma yake akiwa na miaka kama 30.

Lk 3:23 “Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli.” – Alikuwa mwanaume mwenye umri unaotambulika kwamba amekua.

(ii). Mwanakondoo aliangaliwa/alichunguzwa kwa takriban siku tatu.

Kut 12:3,5,6 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.”

Kondoo alichunguzwa kwa siku tatu kwa sababu kuu mbili: Kwanza, kumchunguza kama ana ila (kasoro). Pili, kumpa muda wa kujisafisha

Akigundulika ana ila, anakuwa hafai kwa sadaka. Muda huu alinyimwa chakula ili uchafu wote utoke afae kuokwa (kuroast) akiwa mzima.

Muda wa Kristo tangu kuanza huduma hadi kifo chake ilipita miaka 3 na nusu. Alikufa na kufufuka baada ya siku 3. Mathayo 12:40 “Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.” Hapa tunapata swali jingine la kujiuliza. Je ni kweli Bwana Yesu alikufa Ijumaa? Kama alikufa Ijumaa na kufufuka baada ya siku 3 mchana na usiku, ina maana alifufuka Jumatatu!

Maadui walijaribu kutafuta ‘ila’ kwa Kristo bila mafanikio. Alijaribiwa na shetani akashinda. Alikufa msalabani bila ila wala waa lolote. Akawa Mwanakondoo asiye na ila, Pasaka wetu.

1 Petro 1:19 “bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.”

(iii). Mwanakondoo alichinjwa jioni kuanzia saa 9 kuendelea.

Kut 12:6 “Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.

Sababu ya kumchinja jioni ilikuwa ni ili kila familia iweze kumuandaa mwanakondoo kabla ya giza kuingia.

Kristo (Mwanakondoo wa Mungu) pia alikufa saa 9.

Mk 15:34-38 “Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.”

(iv). Mwanakondoo aliliwa ndani ya nyumba bila kuvunja mfupa

Kut 12:43-46 “Bwana akawaambia Musa na Haruni, Amri ya pasaka ni hii; mtu mgeni asimle; lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla pasaka. Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka. Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; wala msivunje mfupa wake uwao wote.

Kristo (Mwanakondoo wa Mungu) alipokuwa msalabani hakuvunjwa mfupa.

Yn 19:33 “Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu.”

JE PASAKA NI SAWA NA EASTER

Kutoka 20:3-5 “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao.”

Easter ni tamasha la ngono. Jina Easter ama limetokana na Ishtar, mungu wa uzazi wa Mesopotamia, au Eostre, mungu wa kike wa Kijerumani wa majira ya kuchipua.

Dini nyingi za kale zilifanya ibada ya jua, au ngono.

Mayai na sungura siku ya pasaka ni ishara za uzazi za Babeli. Kile ambacho kanisa limefanya hapo ni kuchukua tamasha la kipagani la ngono, ambalo katika kuanzishwa kwake awali katika ibada ya Ishtar lilihusisha kulawitiwa na makasisi wa hekalu pamoja na matendo ya kimila ya ngono na uasherati, na kujaribu kuhusianisha na Yesu.

Jiulize, jinsi gani Mungu anajisikia anapoona kifo na ufufuo wa Mwana wake mpendwa unahusianishwa na ibada chafu ya kipagani ya ngono?

Ikiwa huniamini, ninakuhimiza uangalie asili ya sikukuu hizi. Hakuna siri, ili mradi uwe na nia ya kujifunza bila kutetea historia ya dini na mapokeo ya wanadamu.

Lazima tujiulize kwanini siku ya Pasaka inabadilika kila mwaka. Ikiwa Kristo alifufuka Machi 10, hiyo ingekuwa ukumbusho wa kila mwaka. Lakini niligundua kuwa tarehe ya Pasaka inathibitishwa na unajimu (astrology according to the vernal equinox). Sherehe ya mwanzo wa masika (spring) ya ibada ya kipagani ya jua na majira yaliyofanywa upya iliwekwa pia katika tarehe iyo hiyo. Iliaminika kuwa mungu astarte alianguliwa kutoka kwenye yai kubwa lililoanguka kutoka mbinguni. Druids (waabudu shetani) huko Ulaya walitumia mayai kama ishara za mungu wa kike wa majira ya kuchipua. Sungura inahusishwa na mwezi katika Misri ya kale. Ni ishara ya uzazi.

Kut 23:13 “Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.”

Yos 23:7,8 “Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao; bali shikamaneni na Bwana, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo.”

Ukisoma Catholic Encyclopedia, kanisa katoliki ndilo lilileta mabadiliko haya yote ili yaadhimishwe kwa mtindo wa "Kikristo".  Fuatilia, Easter Controversy (https://www.newadvent.org/cathen/05228a.htm) Katika hatua ya pili ya mabishano ya Pasaka (Easter controversy) kwenye Baraza la Nisea (325 BK). ilikubaliwa kwamba sikukuu ya Pasaka sikuzote ilipaswa kufanywa siku ya Jumapili, na haikupaswa kuwa sanjari na awamu fulani ya mwezi, ambayo inaweza kutokea siku yoyote ya juma, mzozo mpya ulizuka kuhusu uamuzi wa Jumapili yenyewe.

Maamuzi ya Baraza

1. Lazima Pasaka iadhimishwe na watu wote duniani kote katika Jumapili hiyohiyo moja;

2. Jumapili hiyo lazima iwe baada ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa pasaka;

3. Mwezi ule ulipaswa kuhesabiwa kuwa ni mwezi wa pasaka ambao siku yake ya kumi na nne ilifuata ikwinoksi ya masika;

4. Utoaji fulani unapaswa kufanywa, pengine na Kanisa la Aleksandria lililo na ujuzi bora katika hesabu za unajimu, kwa ajili ya kuamua tarehe sahihi ya Pasaka na kuiwasilisha kwa ulimwengu wote (ona Mtakatifu Leo kwa Mfalme Marcian huko Migne, P.L., LIV, 1055).

Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, Tanzania

Please send your love gift to support this ministry. +255 712924234 or CRDB Bank; Account Name: Lawi E. Mshana; Account Number: 0152219784300; Swift Code: CORUTZTZ

 

 





Post a Comment

0 Comments