KANISA LA MUNGU HALINA
WATAZAMAJI (USIYEFANYA LOLOTE KANISANI UNAHATARISHA ROHO YAKO)
Mungu hakukusudia kwamba kanisa lake liwe na watu fulani
ambao wanatumika maisha yao yote (WATUMISHI) kwa ajili ya kundi fulani la watu
ambao wanakuja tu kupokea huduma wanazotoa (WATUMIKIWA). Watumikiwa ni watu
ambao wanakuja tu ibada lakini hawawezi kufanya hata huduma ndogondogo.
Ni kweli kwamba Bwana Yesu hakuwapa waumini wote huduma tano
yaani kuwa mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu. Lakini vilevile
hakukusudia huduma hizo zitumike KUWAHUDUMIA WAUMINI siku zote za maisha yao. Hivi
Mungu anaweza kukuleta duniani ili ufanye mambo yako tu halafu ukiondoka
duniani akuchukue akufute machozi na kukaa na wewe milele? Hawezi kufanya
biashara ya hasara kiasi hicho.
Lazima utambue kusudi la maisha yako na nafasi yako katika
ufalme wa Mungu – kama hujui ufanyeje wasiliana na mimi nikuelekeze usije
ukaipoteza roho yako. Usikubali kuwa mtumishi hewa kanisani kwako.
Kwa mujibu wa Efeso 4:11,12 hizi huduma tano ni kwa ajili ya
KUWAANDAA WATAKATIFU KWA AJILI YA KUMTUMIKIA MUNGU NA KULIJENGA KANISA LAKE. Tumezoea
kusema baadhi ya huduma ni za ndani na zingine ni za nje. Biblia yangu
inaniambia zote zinatakiwa kuzalisha watu kwa ajili ya utumishi. Sio mpango wa
Mungu mtumishi awe wewe tu maisha yako yote.
Efe 4:11,12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.” (And He gave some to be apostles, some prophets, some evangelists, and some pastors and teachers, for the equipping of the saints for the work of ministry, for the edifying of the body of Christ).
Hebu jiulize wewe umemuandaa nani au umeandaliwa kuwa nani na sasa unafanya nini ambacho utaweza kukitolea taarifa siku utakaposimama mbele za Mungu.
Mambo
ya 6 kuzingatiwa na kila mtu anayeabudu na kujiita kanisa:
1. Kila mtu ana karama
(kitendea kazi) fulani aliyopewa na Mungu kwa ajili ya kazi yake.
Hivyo ni wajibu wa kila mtu kugundua karama angalau moja
aliyopewa na kuitumia kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kama hujui tafuta kuijua
maana utaulizwa siku moja. Mungu hawezi kufanya kazi ya hasara ya kukuita umjue
halafu asikupe kazi yoyote.
1 Petro 4:10 “kila
mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili
wema wa neema mbalimbali za Mungu.”
2. Kila mtu azingatie kuitumikisha karama aliyopewa kwa ajili ya
Ufalme wa Mungu (hakuna mtu amepewa karama kwa ajili yake binafsi)
Rum 12:6-8 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”
3. Hakuna mtu aliyejitosheleza kwa kuwa na karama zote. Tumepewa
kwa sehemu hivyo tunahitajiana.
1 Kor 12:14,21 “Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.”
4. Mtu ambaye ni mtazamaji kanisani na hafanyii kazi Neno la Mungu, ni MPUMBAVU na ATAANGUKA KATIKA MAJARIBU
Mt 7:26,27 “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”
5. Mtu ambaye anasikiliza Neno na kuondoka kisha anarudi tena bila kufanya lolote ANAJIDANGANYA (anapoteza muda wake kwa kuwa msindikizaji)
Yak 1:22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”
6. Kila mtu awe mkweli anapotathmini kazi yake kwa Mungu na wala asijidanganye
Wagalatia 6:3-5 “Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.”
Naomba mwaka huu Mungu akujalie kufanya huduma inayogusa wengine ndani na nje ya kanisa lenu ili upate thawabu kwa Mungu.
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe,
Tanga, Tanzania
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)