Ticker

6/recent/ticker-posts

Elimu yako sio mbadala wa uwezo wako


 Elimu yako sio mbadala wa uwezo wako

Wengi wetu tunawekeza katika elimu bila kuitumia elimu hiyo kutusaidia kutambua uwezo tuliopewa na Mungu na namna ya kuuboresha. Kazi kubwa ya elimu ni kutusaidia KUJIGUNDUA na KUJITAMBUA. Kama elimu haitusaidii kujitambua itabidi tusubiri mpaka tukutane na mtu anayeihitaji. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaishi kwa kutegemea huruma za watu badala ya kuishi kwa kutegemea kusudi la Mungu kwetu. Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

Mungu alipomuumba kila mmoja wetu alimpa uwezo fulani ambao haufanani na wa mtu mwingine. Mtu yeyote akiugundua uwezo wa pekee aliopewa lazima atatafutwa na kuhitajika. Kuna eneo ambalo uko vizuri kuliko wote (the best), kuna eneo ambalo umezidi watu fulani (better) na kuna eneo ambalo uko vizuri kama wengine (good). Kama kwa bahati mbaya utawekeza katika eneo ambalo uko vizuri kama wengine, hutakuwa na mvuto mkubwa kwa vile hutaleta tofauti kubwa katika jamii.

Zaburi 139:14 “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana.” Kama ambavyo alama ya dole gumba lako haifanani na mtu yeyote duniani, una kitu ambacho ukiwekeza katika hicho utafanya maajabu. Ukitaka kuleta tofauti, lazima uwe wa tofauti (If you want to make a difference, be different). Wewe ni zaidi ya elimu uliyofundishwa shuleni na ujuzi uliopata chuoni au kwa wanadamu.

Mambo muhimu kuzingatia ili ufanikiwe katika maisha yako:

1. Usikubali kupangiwa maisha na mifumo ya elimu uliyosoma au historia yako.

Waamuzi 6:14-15 “Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.”

Gideoni aliangalia udhaifu wake na historia mbaya ya ukoo wake akashindwa kuona uwezo alio nao. Pamoja na udhaifu aliokuwa nao, alikuwa na uwezo ambao Mungu amempa na Mungu alitaka utumike kusaidia jamii yake.

Kuna kazi nyingi ambazo hujasomea na unaziweza vizuri. Jamii inaweza kuzikubali hata kama huna cheti chake. Jamii haihitaji utambulisho wako bali thamani ya bidhaa au huduma yako. Nadhani maduka unayoenda kununua vitu hujawahi kutafuta kujua wauzaji wana historia gani ya katika maisha yao. Unachojali zaidi ni unafuu na ubora wa bidhaa zao.

2. Kuwa tayari kujifunza jambo jipya kama linahitajika katika soko.

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Mtume Paulo anasema mambo muhimu mawili

(i). Mungu hatamfanyia jambo ambalo amempa uwezo wa kulifanya. Mungu atakachofanya ni kumtia nguvu (empowerment) lakini mtendaji ni yeye mwenyewe (Paulo). Hata Roho Mtakatifu ameletwa kwetu kwa kazi ya kutuwezesha na sio kutufanyia. Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

(ii). Hakuna jambo ambalo Paulo hawezi kulifanya kama atampa nafasi Mungu amuwezeshe. Lazima uamini kwanza kwamba unaweza ndipo utajifunza ili uweze. Mambo mengi unayosema huwezi, hujawahi kujaribu wala kuomba maelekezo ya namna ya kufanya. Ukijiuliza vizuri utagundua kwamba mambo mengi unayosema huwezi hujawahi kuchukua hatua zozote za kupata maelekezo na wewe mwenyewe hujawa kujituma kufanya majaribio kadhaa ili kujiridhisha kwamba huwezi.

Using’ang’ane na vyeti vyako ulivyosoma zamani hata kama ulifaulu sana. Zama hizi za kidijitali kuna mabadiliko makubwa sana. Unaweza kujua sana kompyuta na kukosa fursa kwa vile hujui apps za smartphone. Simu janja na vishikwambi vinatumika zaidi kwa sasa kibiashara kuliko hata kompyuta.

3. Acha misimamo inayomzuia Mungu kukutumia kiupya

Ni kweli kwamba Mungu HABADILIKI lakini ANABADILISHA WATU NA MIPANGO YAKE.

Ukisoma maandiko utagundua kwamba Mungu habadiliki lakini anaweza kubadilisha hali yako na mpango aliokuwa amekupangia kwa sababu mbalimbali. Kama Mungu alikuwa amekuahidi Typewriter mwaka 1965 ukachelewa kuipata, leo atakupa kompyuta.

Yakobo 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.” Ayubu 42:10 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.”

Waliotutanguliwa waliwahi kumpa mpaka Mungu. Zaburi 78:41 “Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.” Hata wewe una tabia ya kutaka kila mtu awe kama wewe na atendewe kama wewe. Mungu hayuko hivyo. Anajua kilicho bora kwa kila mmoja wetu. Mungu anaweza kuumba jambo jipya kwa ajili yako ambalo haliko kwa mwingine.

Mungu akusaidie uweze kujitambua na kutumia vipawa ulivyopewa kwa ajili ya kubadili maisha yako na ya jamii yako.

Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments