Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini tumeacha kusherehekea sikukuu ya Krismasi?


 Kwanini tumeacha kusherehekea sikukuu ya Krismasi?

Huu ni mwaka wa pili tangu tuache rasmi kama kanisa kusherehekea sikukuu ya Krismas. Badala yake kipindi hiki tunakitumia kwa kambi ya maombi ya kufunga (tarehe 24-26 Desemba) kwa ajili ya kuomba rehema na upenyo kwa ajili ya mwaka unaofuata. Haikuwa rahisi. Tulitafuta mistari mingi ya kujitetea lakini tukagundua kwamba hatusomi maandiko tukiwa na lengo la kubadilishwa (open mind) bali tunatafuta kulilazimisha andiko likubaliane na hali zetu na utamaduni wetu. Badala ya kutafuta maana halisi ya andiko (exegesis) sisi tukawa tunatafuta kulifanya andiko likubaliane na tafsiri yetu (eisegesis).

I. Mambo yaliyopelekea kufikia uamuzi huu:

1. Tumejihoji maswali na kupata majibu (soma maswali hapo chini). Muumini wa kweli hafanyi mambo kwa kurithi tu au kwa mapokeo bali inapobidi anahoji ili kujua ukweli wa mambo ili ailinde imani yake. Maandiko yanatuambia kwamba watu wa Beroya walikuwa waungwana kuliko watu wa Thesalonike kwa vile sio tu kwamba walilipokea Neno kwa shauku kubwa bali pia walihoji ukweli wa mafundisho ya mitume wa kipindi chao. Mdo 17:10,11 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”

Kwa vile tumeelewa, tusipotii tutahukumiwa na mstari wa Yakobo 4:17 “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.” Kama umeelewa jambo halafu unajifanya kama huelewi, utahukumiwa.

2. Tumegundua kwamba ingawa tunamcha Mungu wa kweli, tutapotea kama tunaendelea kushiriki ibada za kipagani. Wapo pia waliowahi kumcha Bwana na wakati huohuo wakiendelea kuitumikia miungu na desturi za mataifa. 2 Fal 17:33 “Wakamcha Bwana, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.”

3. Mungu amekuwa akiwafunulia na kuwatuma watumishi wake wengi kipindi hiki kuhusu kuonya kanisa dhidi ya kusherehekea sherehe ambazo zina asili ya kipagani. Ufu 22:18,19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”

II. Maswali fikirishi

Napenda kukushirikisha maswali machache tuliyojihoji tukajiridhisha. HUHITAJI KUGOMBANA NA UJUMBE HUU. KAMA HUU UJUMBE HAUNA MAANA KWAKO WEWE NYAMAZA TU AU UPUUZE. Lakini kuna siku utatakiwa kujibu maswali haya ukiwa peke yako bila msaada wa kiongozi wako.

1.     Je neno Christmas (misa ya Kristo) lina maana ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Kristo?

2.     Je kwanini sikukuu ya Christmas ilianza karne kadhaa baada ya kipindi cha mitume? Nini kilisababisha ianzishwe?

3.     Kama Bwana Yesu na wanafunzi wake hawakusherehekea sikukuu hii, kwanini Wakristo wa leo wanasherehekea? Kwanini Bwana Yesu hakutaja kwamba tuikumbuke siku yake ya kuzaliwa kama alivyotuagiza tuikumbuke meza ya Bwana?

4.     Kwanini Christmas iliwahi kupigwa marufuku kwa miaka zaidi ya 20 katika karne ya 16? Kwanini iliporudishwa tena udhalilishaji mkubwa ulitokea?

5.     Kwanini hata wanaopinga wokovu aliouleta Yesu na kumkejeli na ambao hawako tayari kumpokea mioyoni mwao wanasherehekea Christmas? Mtu anawezaje kusherehekea siku ya kuzaliwa (birthday) ya mtu asiyempenda wala kumuamini?

6.     Kwanini mara nyingi mazingira ya sikukuu ya Christmas yanakuwa hatarishi mpaka polisi waimarishe ulinzi?

7.     Father Christmas (mwenye nguo nyekundu na ndevu nyeupe) ana uhusiano gani na kuzaliwa kwa Yesu Kristo wa Biblia?

8.     Mti wa Christmas au piramidi ya Krismasi vina uhusiano gani na historia ya kuzaliwa kwa Yesu katika maandiko matakatifu?

9.     Tarehe ya Christmas inashabihiana vipi na msimu ambapo wachungaji wa nchi ya Israeli wanakuwa makondeni usiku wakichunga?

 

Wagalatia 6:4 “Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.”


III. Ufafanuzi

 

Mwaka 325 baraza la Nikea lilipitisha sikukuu ya Krismasi ifanyike tarehe hiyohiyo ya sikukuu ya kuzaliwa mungu jua ambayo ni tarehe 25. Wiki la Saturnalia tarehe 17-25 watu waliruhusiwa kufanya maovu bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Mahakama zilifungwa wiki hiyo. Katika karne ya 4 wapagani wengi walisherehekea Krismasi kwa kuahidiwa kwamba wataendelea kusherehekea sikukuu waliyozoea ya Saturnalia.

Kutokana na asili ya Krismasi kuwa ya kipagani, ilipigwa marufuku na Puritans (waumini waliotafuta kulitakasa kanisa la Uingereza liwe la kiprotestanti zaidi) kisha Krismas ikaharamishwa kati ya 1659 na 1681. Ilipohuishwa tena katika karne ya 18 na 19, Wayahudi walidhalilishwa kwa kutembezwa barabarani, kuuawa kinyama, kupigwa hadi kuwa walemavu na wanawake kubakwa.

Neno Krismas halina maana ya kuzaliwa kwa Yesu. Christmas ni kifupisho cha Christ Mass (waliondoa ‘s’ moja lakini ni komunyo takatifu ya Roman Catholic) – desturi ya kanisa la Rumi kwa ajili ya kuivuta dunia kwake, ibada ya sanamu ya kumsulubisha YESU KRISTO tena (the idolatrous recrucifixion). Krismas ni SHEREHE YA KIFO CHA YESU NA KUHAMISHIA UTUKUFU WA UFUFUO WA YESU KWA MUNGU WA KIPAGANI, TAMMUZ. Je, Yesu anahitaji sherehe ya komunyo takatifu (mass)?

Santa Claus (Father Christmas, mwenye ndevu nyingi) ndiye anatangazwa kuliko Yesu Kristo. Kampuni ya Cocacola iliingia mkataba na kuongeza rangi nyekundu. Santa Claus ni mtu wa kumkejeli Yesu. Santa ni anagram ya neno, satan. (Anagram ni neno linalotokana na mpangilio wa neno jingine).

Mti wa Krismas ni mnara wa laana wa mungu wa kipagani anayeitwa Tammuz aliyewakilishwa na mti wa kijani wa kukumbukwa daima (an evergreen, or immortal tree). Yer 10:2-4 “Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka. Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike.” Kum 7:26 “na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.”

Bwana Yesu ametupa maagizo mawili (two ordinances) ya kutenda ambayo ni "Ubatizo" na "Meza ya Bwana". (Rum. 6:3-5, Kol. 2:12, I Kor. 11:17-34). Sherehe ya Krismasi haina msingi wa kimaandiko. Desemba hadi Februari ni miezi ya baridi sana Israeli kutegemea wachungaji wawe na mifugo yao porini au Yusufu kuweza kusafiri. (Lk 2:8,9).

Zakaria, alikuwa kuhani wa zamu ya Abiya. (Lk 1:5). 1 Nya 24:6-10 “…ya saba Hakosi, ya nane Abia.” Zamu ya Abiya ilikuwa kuanzia katikati ya Mei hadi katikati ya Juni.

Lk 1:24-28 Mwezi wa sita (Kislev, Desemba) malaika Gabrieli akatumwa kwa Mariamu. Hivyo Yesu alizaliwa miezi 9 baadaye (Tishri, mwezi Septemba). 

KUFANANA KWA ‘SATURNALIA’ NA ‘KRISMASI’

Watu walipumzika kufanya kazi zote. 2. Watumwa (waajiriwa) walipewa uhuru wa muda mfupi. 3. Vizuizi vya kimaadili vililegezwa; hata watoto waliruhusiwa kunywa pombe. 4. Zinaa ilifanyika kama njia ya kutoa zawadi. 5. Kiti cha mfalme wa dhihaka (Good Ole Santa) kinainuliwa madukani. 6. Wimbo wa "I O Saturnalia" ulisikika kila mahali. Wimbo wa Merry Christmas unasikika kila mahali. 7. Miti ya kijani kibichi ilitumika kwa kupamba (ishara za kuzaliwa upya (rebirth) na uwezo wa kuzaa (fertility)). 8. Nguruwe wa kiume aliuawa na kuliwa (ishara ya Frey, mungu wa kuzaliwa upya (god of regeneration)). Je, nguruwe sio nyama kuu wakati wa Krismas? 9. Keki (Yule log) inayoandaliwa kama ishara ya maisha yanayoendelea (continuing life). 10. Taa zinatumika kuondoa giza linaloongezeka msimu wa baridi.

Kwa hiyo sikukuu ya kipagani ya Saturnalia ikawa ndiyo Krismasi

Maandiko mengine ya ziada:

2 Kor 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”

Kum 11:16 “Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu.”

Law 18:30 “Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

Kut 20:3-6 “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.

Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255712924234, Tanzania

Post a Comment

0 Comments