Ticker

6/recent/ticker-posts

Maswali na Majibu kuhusu Utoaji (sehemu ya kwanza)


 Kipindi cha Maswali na Majibu kuhusu Utoaji tulichofanya Jumapili jioni

Nashukuru sana kwa kanisa lililonikaribisha kuhudumu Jumapili nikiwa katika umisheni Nyanda za Juu Kusini ambapo jioni tulikuwa na kipindi maalum cha Maswali na Majibu kuhusu Utoaji.

Napenda kukushirikisha maswali kadhaa niliyoulizwa maana inawezekana hata wewe una maswali kama hayo. FOLLOW huu ukurasa ili uendelee kupata taarifa.

Haya maswali ambayo niliulizwa nitayajibu hatua kwa hatua:

1.     Kwa nini watu wanashindwa kumpa Mungu 10% (zaka) ya mapato yao wakati Mungu hakusema tugawane nusu kwa nusu anapotubariki?

2.     Ninajisikia uchungu wakati ninapotoa zaka. Lakini nikishatoa najisikia amani. Hii ina maana gani?

3.     Kama nimetumia laki 1 kununua mfugo halafu akakua na nikamuuza kwa laki 3, natoza zaka shilingi ngapi?

4.     Je, nikiokoka natakiwa kutoa zaka ya mali nilizokuwa nazo kabla sijaokoka?

5.     Kuna mtu amekuwa akiniombea na kunishauri kwa njia ya mtandao. Sasa ameniambia nimtumie sadaka ya shukrani. Je, nimtumie?

6.     Je ni lazima nitoe malimbuko ya kila shamba langu au naweza kutoa malimbuko kutoka shamba moja tu?

7.     Ni sawa kutoa sadaka kama mbegu katika madhabahu ya Mungu kwa mahitaji maalum zaidi ya utoaji wa siku za ibada?

Leo naanza kukupa majibu ya swali namba 1 na 2.

1.     Kwa nini watu wanashindwa kumpa Mungu 10% (zaka) ya mapato yao wakati Mungu hakusema tugawane nusu kwa nusu anapotubariki?

2.     Ninajisikia uchungu wakati ninapotoa zaka. Lakini nikishatoa najisikia amani. Hii ina maana gani?

Zipo sababu kadhaa zinazosababisha watu washindwe kutoa zaka (10%) ya mapato yao au watoe zaka kwa uchungu:

1.     Kuna watu wanadhani wanapotoa zaka wanampa mchungaji wao au dhehebu lao. Wanadhani wanamnufaisha kiongozi wao. Hawajui kwamba wakati mtu anapotoa zaka anapaswa kujiona kwamba anampa Mungu na sio kiongozi wake. Andiko halisemi leteni zaka kamili katika NYUMBA YA MCHUNGAJI bali katika NYUMBA YA MUNGU. Zaka ni agizo la Mungu na sio la mchungaji wala dhehebu. Malaki 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.”

2.     Kuna watu wanadhani wanapotoa zaka wanamsaidia mchungaji wao. Hawajui Mungu ndiye anampa kiongozi na sio wao waliotoa. Hivyo wakiwa na chuki binafsi na Mchungaji wao wanadhani wanamuadhibu kwa kutotoa zaka (wanadhani wanapogoma kutoa zaka mchungaji atatambua hasira yao). Ukiona mshirika anasema mchungaji amenikwaza sana hivyo sitatoa zaka yangu ujue huyo zaka yake haijawahi kutambuliwa na Mungu. Ukitaka KUMSAIDIA Mchungaji wako msaidie katika pesa uliyobaki nayo baada ya kutoa zaka. Hapo ndipo utapata thawabu ya kumsaidia. Unapotoa zaka unampa Mungu na sio mchungaji wako. Unatakiwa kumshirikisha mchungaji au mwalimu wako baraka zako baada ya kutoa zaka. Wagalatia 6:6 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.”

3.     Kuanza kutumia pesa kabla ya kuitolea zaka kunamfanya mtu baadaye aone kwamba haitoshi. Hivyo ni rahisi kuona uchungu wakati anapotoa. Tambua kwamba Mungu anataka tutoe zaka (asilimia 10) YA KWANZA na sio asilimia 10 ya mwisho. Hivyo mtu akipokea tu pesa anapaswa kutenga zaka (10%) ndipo aanze matumizi binafsi hata kama siku ya kuipeleka kanisani haijafika. Mungu anaangalia utoaji wa zaka mara tu mtu akishapokea baraka na sio wakati wa kuipeleka kanisani. Kumbuka zaka inapocheleweshwa au kukopwa inatakiwa kuongezwa sehemu ya 5 sawa na 20%. Law 27:31 “Na kama mtu akitaka kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake.”

4.     Wengine wanadhani wana mamlaka ya kupangia matumizi ya zaka. Ni dhambi kwa muumini kupangia matumizi ya zaka. Ni rahisi watu kukushukuru unapowasaidia kwa kutumia zaka lakini kwa kufanya hivyo unampora Mungu nafasi yake yaani, unachukua nafasi ya Mungu. Unapaswa kusaidia watu kwa kutumia asilimia 90 uliyobaki nayo baada ya kutoa zaka. Unakaribisha laana pale unapokuwa na vitakatifu katika nyumba yako. Kum 26:13 “nawe sema mbele ya Bwana, Mungu wako, Vitu vilivyo vitakatifu nimeviondoa katika nyumba yangu…”

5.     Wengine wanadhani zaka (10%) inaweza pia kutumika kusaidia wageni, yatima na wajane. Unapaswa kujua kwamba 10% ya kwanza ilisaidia Walawi (Hes 18:21,24), zaka ya pili ni ya Sikukuu (Kum 14:22-27) na ya tatu katika mwaka wa tatu waliongeza 10% kwa ajili ya hayo makundi mengine (Majirani). Ukitaka kutumia zaka kusaidia maskini unatakiwa kuongeza ifikie asilimia 30%.  Kum 26:12 “Utakapokwisha kutoa zaka, katika zaka zote za maongeo yako mwaka wa tatu, ambao ndio mwaka wa kutolea zaka, umpe zile zaka Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, wapate kula ndani ya malango yako na kushiba.” Sisi tunaendelea na hii zaka ya ukuhani wa Melkizedeki ambayo ni asilimia 10 (10%).

6.     Wengine wamesikiliza na kuamini mafundisho potofu ya watu wasiojua Biblia vizuri au wanaoipotosha kwa makusudi. Kuna watu wanasema zaka ilikuwa kipindi cha sheria na wengine wanasema Agano Jipya halijaelekeza kutoa zaka.

(a). Abramu alitoa zaka KABLA ya kipindi cha sheria. Mwanzo 14:20 “Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”

(b). Yesu alitaja zaka katika kipindi cha Agano Jipya na hakusema watu waache kutoa zaka. Bali alisema watangulize mabadiliko ya kiroho. Luka 11:42 “Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.” Waebrania 7:8 “Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai.”

Kumbuka ku-FOLLOW huu ukurasa ili uendelee kupata taarifa za majibu ya maswali yaliyobaki.

Mungu atuwezeshe kutii Neno Lake kwa ajili ya usalama wetu wa sasa na wa milele.

Dr Lawi Mshana, +255 712-924234

Post a Comment

0 Comments