Ticker

6/recent/ticker-posts

Umeombewa na mtumishi mwenye mafuta (upako) gani?

UMEOMBEWA NA MTUMISHI MWENYE MAFUTA (UPAKO) GANI? UNAJUA YAPO MAFUTA YA KISHETANI? 

Ni kweli usiopingika kwamba mafuta yametumika hata kipindi cha Biblia kumuwakilisha Roho Mtakatifu kwa ajili ya kuwafungua watu katika matatizo mbalimbali. Hata Bwana Yesu mwenyewe alitumia mafuta katika kuponya wagonjwa. Isaya 10:27 ‘Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.’ Mk 6:13 ‘Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.’ Yakobo 5:14 ‘Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.’ Lakini shetani hupenda kujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 2 Wakorintho 11:14,15 ‘Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.’ Inawezekana umenaswa na watumishi hao ndo maana huoni makosa yao. Unaposhiriki dhambi zao utashiriki na mapigo yao. Ufu 18:4 ‘Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.’ 

Ngoja nikutajie baadhi ya majina ya mafuta wanayotumia na kazi zake: 

1. ‘DO AS I SAY’ – Mafuta haya yanawafanya waumini wao kufanya chochote wanachoagizwa bila kuhoji. Wanafungwa fahamu kiasi kwamba hata kama wanachoagizwa kinapingana na Neno la Mungu wao wanakubali tu. Kimsingi wanamuabudu kiongozi wao badala ya kumuabudu Yesu Kristo. Wanamuweka kiongozi wao katika nafasi ya Mungu asiyekosea (infallible) 1 Pet 2:22. 2. 

‘ALL SEEING OIL’ – Mafuta haya yanamsaidia mtumishi huyo kuona siri za ndani za mtu. Watu wengi wakitajiwa mambo ya ndani ya maisha yao wanaona kwamba lazima ni ufunuo wa Mungu aliye hai. Pepo la uaguzi linaweza kuona na kusema ukweli kwa malengo kwamba uliamini ndipo baadaye lianze kukudanganya. Mdo 16:16-18 ‘Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.’ Kama Mtume Paulo hangekuwa na karama ya kupambanua roho angedanganywa na pepo la uaguzi (spirit of divination) kwa vile lilichokisema kina ukweli. Tusiangalie tu ukweli, bali pia tuangalie chanzo cha taarifa. 

3. ‘SLAYING OIL’ – Mafuta haya yanamsaidia mtumishi kuwaangusha watu kwa maonyesho tu na sio kwa nguvu yenye malengo ya ki-Mungu. Watu wanaweza kuangushwa lakini hakuna badiliko lolote katika matatizo waliyo nayo. Hata hivyo kuna wakati Mungu anaweza kujidhihirisha kipekee kwa watu wake mpaka washindwe kusimama. 2 Nya 5:14 ‘hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa Bwana.’ 

4. ‘CROWD PULLING OIL’ – Mafuta haya yanawafanya waweze kuvuta makusanyiko makubwa ya watu kwa kipindi kifupi. Na kwa vile kipimo cha kukua kwa kanisa kwa wengi ni kiidadi tu (numerical growth) na sio kiroho (spiritual growth) wala kiuchumi (economic growth), wananaswa. Watu wanaweza kuwa wengi lakini ni wachache sana wanaojua kuomba na ni wachache sana wana hali nzuri kiuchumi. Wengi wanakamuliwa tu huku wameshindwa kupata milo mitatu kwa siku na wameshindwa kupeleka watoto wao shule na bado ni washabiki wazuri wa imani yao. 

5. ‘TOUCH AND FOLLOW’ – Mafuta haya yanamsaidia mtumishi kupumbaza akili za watu (hypnotize) wamfuate na kufanya mambo maovu bila kujitambua. Mfano, wanaweza kuwanasa wake za watu au waume za watu kwa kiasi ambacho wanazini nao bila kuona kwamba wanatenda dhambi. Na wakishatenda dhambi shetani anaweka maneno ya unabii katika vinywa vyao. Yupo aliyesema alipokuwa katika utumwa huo kwamba, alitakiwa azini na bikira au mke wa mtu na akimaliza tu aende moja kwa moja madhabahuni kuhubiri bila kuoga. Watumishi hawa wana kiapo cha siri. Na kwa vile wamefanya maagano, kama watatoa siri bila kuombewa na mtumishi wa Mungu mwenye mamlaka ya kuvunja madhabahu za kishetani, wanaweza kufa. Mkazo mkubwa wa ujumbe wao ni mafanikio (prosperity) na wanatakiwa kuepuka jumbe kuhusu ‘wokovu na haki’. Hata hivyo sio vibaya kufundisha kuhusu mafanikio ikiwa mafundisho hayo yanatolewa katika msingi wa ki-Biblia na kwa uwiano mzuri na masomo mangine. Sehemu ya zaka inayotolewa katika huduma hizo inatakiwa kumfikia shetani. Ndugu zangu, tusitafute njia za mkato katika kufanikiwa.Biblia imetuonya sana. Lk 9:23-25 ‘Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?’ Pamoja na kwamba shetani atajitahidi kuiga kazi za Mungu, bado nguvu ya Mungu itafunika. Kut 7:11,12 ‘Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.’ Nakusihi wewe uliye kwenye kifungo cha aina yoyote na umeshindwa kujinasua uwasiliane nasi ili tukushauri na kukuombea. 

DAMU YA YESU KRISTO ILIYOMWAGIKA MSALABANI KWA AJILI YA UKOMBOZI, IKUTOE KATIKA MAAGANO HAYO. UWE HURU KATIKA JINA LA YESU KRISTO ALIYE HAI!“ 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments