Siku 5 Mbinguni na Kuzimu (Safari ya pili) – Bernada Fernandez
Jiandae kwa kurudi kwa Bwana Yesu! Siku 5 Mbinguni na Kuzimu
Habari unayokwenda kuisoma, ni safari ya pili ya ushuhuda wa dada Bernarda Fernandez, ambaye alipata bahati ya kuchukuliwa na Bwana Yesu Kristo kutembelea ulimwengu ujao.
SAFARI YANGU YA PILI
Siku moja tulikuwa kwenye kipindi cha maombi, tulikuwa ishirini. Kama kawaida tulianza kumsifu na kumwabudu Bwana. Ghafla tulihisi uwepo wa Mungu. Kulikuwa na nguvu za Mungu kama siku ile ya Pentekoste. Nakumbuka mama mkwe, ambaye umri wake ni mkubwa sasa na aliyejitoa sana kwa kazi ya Mungu alikuja kwangu na kuniambia: "Bernarda, hebu tupunguze sauti zetu wakati wa kusifu kwani sauti zetu ziko juu sana". Ni kweli alikuwa sahihi, kwani kusifu kwetu kulikuwa kama maji mengi yanayomwagika. Nikiwa najiandaa kuwaomba kaka zangu kupunguza sauti, Nilimsikia Bwana Yesu akiniambia: "Usiwaambie cho chote! Mtaani, watu wanapopiga kelele hakuna mtu ye yote anayejali, kwanini ninyi muache kusifu kwa nguvu?" Kisha tukaendelea kumsifu na kumwabudu Mungu, na nilijisikia kama kuna jambo kubwa linaenda kutokea. Ghafla nilikumbuka kile Bwana alichoniambia katika safari yangu ya kwanza: "Nitarudi tena kwako".
Mara nikaona mwanga mkubwa uliomulika nyumbani kwangu. Kaka zangu pia waliuona huo mwanga, na wote walipiga magoti mbele ya huyu aliye Mungu wa Kweli na Mwaminifu. Sikujua la kufanya, nilibaki nimesimama. Mwanga ukawa mkali zaidi, na kubadilika kuwa umbo la mwanadamu. Mbele yangu alikuwa Bwana Yesu Kristo ambaye kuangalia kwake kulikuwa kuzuri sana kulikojaa upendo. Hapa duniani sijawahi kamwe kuona mtu mwenye sura nzuri kama hiyo. Akasogea karibu na kila mmoja wa kaka zangu. Nilipokuwa nataka kuwaambia kaka zangu kuwa Bwana amekuja kwa ajili yangu nilianza kunena kwa lugha. (1 Korintho 14:39-40)
Bwana alisogea karibu yangu. Kwa kuniangalia tu, roho yangu iliachana na mwili wangu. Nilikuwa hewani na kuona kile kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwangu. Niliona watu wakipiga kengele iliyokuwa mlango, mume wangu, alipotoka kuangalia, alikutana na polisi wawili wakiwa mlangoni. Polisi hawa walisema: "Tumesikia kuna mwanamke amefariki hapa ndani ndio maana tumekuja". Mume wangu akawajibu na kuwambia hapana, hapa tunamwabudu na kumsifu Mungu. Wale polisi hawakuamini, lakini hawakuweza kuingia ndani. Walisema: "Sawa, endeleeni lakini msipige kelele kubwa". Nilikuwa angani wakati naona haya yote.
Bwana Yesu alinishika mikono yangu na tukawa tunaelekea Nchi ya Jamhuri ya Dominica. Tulipofika kwenye jiji, Bwana aliniambia: "Hapa kuna aina mbili kubwa za dhambi zinazofanyika mbele za Baba yangu, Uchawi au ushirikina na kuabudu miungu (sanamu)". Niliona watu wa nchi ile wakikimbilia kwa wapiga ramli na wanaoonyesha mazingaombwe...
Baada ya hayo Bwana akanileta katika nchi ya Venezuela na nchi ya Mexico. Katika nchi hii ya Venezuela, nikiwa angani na Bwana Yesu, niliona watu wakigeukia ushirikina, mazingaombwe na uganga wa kienyeji. Katika nchi ya Mexico niliona watu wakiwa kwenye makundi wanaabudu mapepo. Bwana akaniambia: "Kilio cha dhambi hii kimefika kwa Baba yangu. Ishara ya kwanza ninayoitoa kama onyo ni kwamba kutakuwa na tetemeko la nchi katika nchi hii ya Mexico kama wananchi wa nchi hii hawatatubu na kunirudia mimi". Niliporudi tu duniani, nilipeleka ujumbe huu kwa nchi ya Mexico. Watu wa Mexico hawakujali ujumbe huu na hivi karibuni kulitokea tetemeko la kutisha katika nchi hii ya Mexico.
Wakati bado tukiwa angani, Bwana aliniambia kwamba mikono ya Baba yake imenyoshwa juu ya watu waishio duniani. Niliona bahari ikiwa na mawimbi makubwa kama jitu la kutisha Pia niliona kimbunga kikubwa kinatokea duniani. Nilimuuliza Bwana: "Bwana kutatokea nini kwa Watu waliookoka mambo haya yakitokea?" Alinijibu: "Nenda kawaambie kwamba, kwa wale waaminifu kwangu, hakuna hata unywele utakaouguswa".
Baada ya hayo Bwana alinipeleka mahali pengine, Niliona mahali nchi inapasuka vipande vipande. Bwana akaniambia: "Nchi nyingi karibuni zitafutika". Kisha tukaondoka mahali pale na kwenda mahali pengine ambao maji yalikuwa yanatembea. Tulipelekwa na maji haya kupitia ndani ya handaki nakufika chini kabisa ya dunia. Niliona malango makubwa. Haya yalikuwa tofauti na yale niliyoyaona katika safari yangu ya kwanza. Katika malango haya kulikuwa na minyororo mikubwa. Bwana alienda katika malango haya baada ya kuondoa minyororo, akaniruhusu kuingia ndani kupitia katika handaki.
Ndugu wapendwa, Niliona maelfu ya watu, wakiwa wameinamisha vichwa chini, wamevaa nguo zilizoraruka raruka. Walikuwa wamefungwa kwa minyororo mikubwa ambayo ilikuwa ikitoa sauti kali ambayo inaweza kumfanya mtu kuwa kiziwi. Kisha nikauliza: "Bwana hii ina maana gani?" Alinijibu: "Wanaume na wanawake hawa wako njiani kuelekea kuzimu". Miongoni mwa watu hawa ambao wanaelekea kuzimu, nilimwona kaka mkubwa wa mume wangu (shemeji yangu), Adolfo. Alikuwa mtu mjeuri, alikuwa anaoa na kuacha kama anavyotaka na alikuwa amezoea kumtukana Mungu. Kisha nilianza kumsihi Bwana anipe nafasi nirudi duniani kumwonya Adolfo kwamba asipojirekebisha anaenda kuzimu, lakini Bwana hakunijibu. Nikawaona tena Adolfo na mkewe wanatembea kupitia katika lile handaki. Walikuwa pembeni kabisa mwa kuzimu. Nilimsihi tena Bwana aniruhusu nirudi duniani nikawaambie watu yale niliyoyaona. Bwana akainua mikono yake na kusema: "Nenda na waambie kuwa muda karibu kabisa unakwisha". Alisema tena: "Maelfu kwa maelfu ya watu watakwenda kuzimu, muda wa Adolfo umekwisha anakwenda kufa muda mfupi sana ujao".
Baada ya kurudi duniani na kumweleza shemeji yangu Adolfo, hakutaka kubadilisha njia zake za maisha. Siku moja, alirudi haraka nyumbani kutoka kazini na kumwambia mkewe: "Siwezi kuifanya kazi tena, kwani kuna kitu kinaniambia kuwa nitakufa". Mkewe akamjibu: "Ni kwasababu umelewa kama kawaida yako ndio maana unasema hivyo". Wote baadaye wakaenda kulala. Baada ya dakika kadhaa mkewe akaona maono. Katika maono haya alijiona yeye na mumewe katika handaki, wakiwa wamevaa nguo zilizoraruka raruka na walikuwa wanaelekea kuzimu. Alisikia sauti kutoka kwa Bwana Yesu ikimwambia: "Muda wenu umekwisha".
Wakati nikiwa bado hewani Bwana aliniambia: "Unajua ni kwanini nimekuleta hapa kwa mara ya pili? Ni ili nikuonyeshe kwamba wakati ulipokuja hapa mara ya kwanza, watu waliotupwa kuzimu walikuwa wachache kulinganisha na wakati huu".
Ghafla Bwana Yesu na mimi tuliondoka mahali hapo na kwenda mbingu ya kwanza, na baadaye ya pili. Tulipofika mbingu ya tatu, niliona malaika wakiwa na shughuli nyingi huku na kule; kisha nikamuuliza Bwana: "kwanini malaika hawa wanakimbia huku na kule?" Bwana Yesu akajibu: "Ni kweli malaika wangu hapa wanakimbia huku na kule, lakini nakwenda kukuonyesha jinsi pia duniani kulivyo na kukimbia huku na kule. Uwe mwangalifu kwani mapepo mengi yameivamia dunia. Ibilisi ana hasira sana juu wa watu Waliookoka kwa vile ana muda mchache tu uliobaki".
Bwana akaniruhusu kuyaona hayo mapepo yenye hasira, na akaniambia: "Hayo mapepo unayoyaona ni mapepo ya zinaa. Yatawashambulia maelfu ya watumishi wangu na wengi wataanguka katika dhambi ya zinaa. Unajua ni kwanini ibilisi anafanikiwa kuwaangusha watumishi wangu? Ni kwasababu watumishi wangu hawanipi Mimi utukufu wangu wote. Wanaiba utukufu wangu na kuwa na kiburi. Pamoja na hayo wake zao wanaishi maisha yasiyo na mpangilio mzuri wa kiroho. Hawajengi nyumba zao kwa hekima." (1 Timotheo 2:11-14)
Niliona maelfu ya malaika ambao sikuweza kuwahesabu, wengi miongoni mwao walikuwa tayari kwa vita. Kisha Bwana Yesu akaniambia: "Sasa nawatuma maelfu ya malaika hawa duniani kulinda watu wangu. Katika siku hizi za mwisho, nitaweka ulinzi mara mbili, shetani naye ataongeza mashambulizi mara mbili, lakini usisahau kwamba Mungu wako ni Mungu Mkuu sana na Mwenye Uweza wote. Kama uko ndani Yake hakuna kitakacho kudhuru".
Kisha Bwana akanipeleka sehemu nyingine. Hapa, niliona meza kubwa iliyozungukwa na viti vya dhahabu. Kila kiti kimeandikwa jina la mtu, na vazi la kitambaa kizuri sana liliwekwa pia juu ya kila kiti. Mbele ya kila kiti, juu ya meza niliona taji. Niligundua kwamba kulikuwa na kiti kimoja ambacho kilikuwa kikubwa kuliko viti vingine vyote. Mbele ya kiti hiki kikubwa kulikuwa na kikombe kikubwa cha dhahabu. Bwana Yesu akaniambia niende nikachungulie kwenye hicho kikombe nione kilichomo humo. Ilikuwa ni divai ambayo ilikuwa tayari kugawiwa watu. Bwana Yesu akaniambia: "Unafahamu ni kwaninini divai iko tayari kugawiwa watu? Nenda waambie watu wangu kwamba niko mlangoni, nakuja sasa".
Bwana akanipa vazi zuri sana na taji. Nikalivaa pamoja na ile taji, kisha Bwana akanipeleka mahali pengine ambapo niliona vitu kama kwenye kioo. Aliniambia: "Hakuna doa wala wala kunyanzi kwenye vazi lako, si ni kweli? Hakuna ye yote atakayeingia kupitia mlango huu wala kukaa katika meza hii, isipokuwa amevaa vazi kama hili. Baadhi ya watu wangu walioko duniani wamechafua mavazi yao. Wengine wamekunja kunja mavazi yao, na wengine zaidi wameyavua kabisa mavazi yao na kuyaweka pembeni na kuyasahau kabisa. Waambie watu wangu kuwa huu ni wakati wa kuyafua mavazi yao kuyapiga pasi na kuyavaa tena. Watu Waliookoka ni lazima kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kuyatunza mavazi yao katika hali nzuri, kwa kuwa muda mfupi sana ujao Mfalme atasherehekea Karamu ya Harusi katika ufalme wa Baba yangu".
Mimi natoka katika familia ya kutalikiana (kuachana) na nililelewa na baba tu. Mama yangu alikuwa mtu wa dini ya kipagani. Wakati baba yangu, alikuwa haamini cho chote. Nilikuwa na dada yangu ambaye alikuwa katika makundi ya walevi, lakini najua kuwa ni muda mfupi tu ujao Bwana Yesu atamtoa huko kwenye ulevi na tutahubiri pamoja Injili. Ninamwombea sana. Wakati nilipokuwa nafikiri maisha ya mama yangu katika dini yake ya ajabu aliyokuwa nayo, wakati wa safari yangu ya kwanza paradiso, nililia sana mbele za Bwana Yesu na kumwambia: "Bwana mama yangu amepotea, nimejaribu sana kumhubiri injili lakini hataki kusikiliza. Bado ameshikilia dini yake ya kipagani". Bwana akanijibu: "Nitamwokoa mama yako, lakini nitamchukua nyumbani mara tu baada ya kuokoka vinginevyo atarudi dhambini na kwenda kuzimu. Kwa sababu hii, mara tu baada ya kuokoka muda mfupi baadaye atakuja hapa paradiso".
Niliporudi duniani, niliomba, nililia, kuomboleza kumkumbusha Bwana ahadi yake aliyonipa, lakini nilimwona mama yangu bado akiendelea na ibada ya sanamu katika dini yake. Siku moja Mungu alimtumia kijana wangu kumbadilisha mama yangu. Siku tatu tu baada ya mama yangu kuokoka, akafariki; Bwana asifiwe!
Wakati wa safari yangu ya pili paradiso Bwana aliniambia: "Angalia, kile ambacho kinywa changu kinanena, mikono yangu hukitimiza". Nilimwona mama yangu pale mahali pazuri paradiso; alikuwa miongoni mwa wamama. Kisha Bwana akaniongoza kwenda mahali pengine katika paradiso. Pale niliwaona maelfu ya watoto wadogo waliovalishwa nguo nyeupe wakiwa wanamsifu na kumtukuza Bwana. Bwana akaniambia: "Watoto hawa ni wale waliotolewa mimba na mama zao na madaktari waovu.
Watoto waliouwawa wakati bado wakiwa tumboni mwa mama zao, na wale waliotupwa kwenye mashimo ya takataka na kwenye mito, wako hapa mbinguni."
Ndugu mpendwa, tofauti na unavyofikiri, kwa Bwana mimba ikishatungwa kuanzia siku ya kwanza tu ni kiumbe halisi (ni mwanadamu kamili).
Bwana Yesu akaniambia tena: "Bernarda, fanya kazi yangu kwani Mimi ndiye nguvu yako. Ujumbe huu ni muhimu uufikie ulimwengu wote. Huu ni ujumbe kwa Waliookoka, wachungaji, na watu wote wakaao juu ya uso wa dunia ikiwa ni pamoja na wewe. Mtakatifu na azidi kutakaswa."
Wakati huu malango ya mbinguni yakafunguliwa. Kulikuwa na hali ya utukufu mkuu. Bwana Yesu akawaita maelfu ya malaika ambao walikuwa mahali hapo, kisha Bwana Yesu akanisindikiza kuelekea nyumbani duniani.
Wakati tuliporudi nyumbani, nilimuona mume wangu na wapendwa wengine Waliookoka waliokuwa wanasubiri roho yangu irudi katika mwili. Niliuangalia ule mwili wa nyama uliobaki duniani, na kumwambia Bwana kwamba siutaki tena mwili huu. Bwana akanijibu: "Huwezi kwenda mbinguni na mimi kwani muda wako bado haujafika. Ni lazima uwaambie kwanza watu wangu yale uliyoyaona ili wawe tayari". Kwa sauti yenye mamlaka, akaniambia: "Ingia katika mwili huo, na upokee uzima,, Mimi ndio huo ufufuo na uzima, ye yote anayeniamini, ajapokufa, atakuwa anaishi (Yohana 11: 25-26).
Kutoka kwa dada Bernada Fernandez
JINA LA BWANA LIBARIKIWE!
NENO LA BWANA LIBARIKIWE!
KAZI ZA BWANA ZIBARIKIWE!
NJIA YA BWANA IBARIKIWE!
Roho Mtakatifu na autumie ushuhuda huu kusema na wale wote ambao kweli WANATAFUTA KWELI YA MUNGU; MAPENZI YA MUNGU; NJIA ZA MUNGU—USO WA MUNGU; MUNGU MWENYEWE.
AMEN.
MWENYE MASIKIO NA ASIKIE!
Unaweza ku-share ujumbe huu kwa wengine na kutoa maoni yako.
Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)