NINI MAANA YA KUIBIWA NYOTA KWA MUUMINI WA KWELI (Sehemu ya kwanza)
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba watu wengi wameanza kusikia kuhusu nyota kwa wanajimu na wachawi na sio kwenye Neno la Mungu. Hivyo wanadhani shetani ndiye aliyeanzisha nyota wakati yeye hamiliki kitu zaidi ya kuibia watu na kuhamishia kwa wengine.
Yapo maandiko mbalimbali ambayo yanazungumzia nyota kwa mtazamo mzuri. Nilishirikisha katika somo lililopita kwamba mamajusi waliiona nyota ya ufalme wa Bwana Yesu alipozaliwa na sio kila mtu aliiona. Mt 2:1,2 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Shetani kabla ya kuanguka alikuwa ‘nyota ya alfajiri’. Isaya 14:12 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!”
Ufu 12:1 “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.” Katika andiko hili taji ya nyota 12 inawakilisha ‘nuru na uongozi wa mitume kumi na wawili.’
Ufu 1:20 “Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.” Katika andiko hili nyota zinawakilisha watumishi wa Bwana Yesu.
Watu ambao wanaujua ulimwengu wa roho hata kama ni watumishi wa shetani wanaweza kuona nyota ya mtu. 1 Sam 28:11-13 “Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli. Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi.”
Tuna watu wengi leo wameibiwa mng’ao wa mafanikio yao (nyota) na kufanywa mateka (misukule). Wananufaisha wengine lakini wao wenyewe wako hoi. Isaya 42:22 “Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.”
Hata katika watu wa Mungu sio wote wamejaliwa kujua ngazi za ulimwengu wa roho. Yapo mambo katika ulimwengu wa roho ambayo hayaelezeki kwa lugha ya hapa duniani. Paulo aliwahi kusema kuhusu hili alipofika mbingu ya tatu. 2 Kor 12:2-4 “Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.”
Mfano katika huduma ya maombezi ninayofanya nimekutana na watu waliookoka ambao wanateseka tu kwa vile waliibiwa kitovu na wachawi wakati wanazaliwa. Najua utasema kiliibwaje, kiko wapi na kitarudishwaje? Haya yanatambulikana kwa jinsi ya rohoni. 1 Wakorintho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” Kwa hiyo hata kama umeokoka unaweza usinielewe kama hujawahi kuingia zaidi katika ulimwengu wa roho (spiritual realm). Ila ukweli utabaki palepale kwamba kama sio wewe wapo watu wamepigika hata kama wana bidii katika mambo mengi bila sababu za msingi.
Nyota ina maana ya hatima yako inayong’aa (a colourful destiny). Shetani akizima mng’ao wako, mwisho ni maisha ya hasara.
Umeumbwa kuleta ufumbuzi fulani hapa duniani: Yer 1:5 “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”
UNAWEZA KUIBIWA NYOTA WAKATI GANI?
1. Ukiwa tumboni mwa mama yako
2. Wakati wa kuzaliwa (hasa kupitia wakunga ambao ni waabudu shetani)
3. Ukiwa umeshazaliwa (tangu utoto wako hadi sasa)
Mtu aliyeibiwa nyota anakuwa na sifa za mafanikio kwa nje lakini katika uhalisia hakuna kitu. Anayestahili kuwa juu anakuwa chini, halafu mpumbavu ndiye anakuwa juu badala yake. Mhu 10:5-7 “Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye; ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.”
Shetani anaweza kuleta uharibifu kabla mtu hajamjua Mungu. Lakini pia anaweza kuleta uharibifu mtu akiwa anamjua Mungu kama atampa nafasi (mlango wazi). Kama hili halingewezekana mtu akiamini, hatungekuwa na watu wa Mungu wenye maisha magumu na madeni yasiyolipika wakati Bwana Yesu ametulipia deni zetu zote msalabani. Mt 13:24-29 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo.”
Ushuhuda hai:
Mama fulani aliyeokoka wakati amejifungua mtoto akasikia mkunga mmoja kati ya watatu akimwambia mwenzake, “Kwanini unataka kuchukua kila kitu. Humuachii hata moja huyu mtoto masikini! Akaendelea kusema, umefanyia watoto wengi wasio na hatia na umekuwa hutupatii mgawo sawa. Nitaweka wazi jambo hili.” Kisha akamwambia yule mama mzazi, “Mtoto wako ana nyota 7 na huyu mama (mkunga mwenzangu) amechukua nyota 6 na sasa anachukua ya 7. Hii sio sawa. Angemuachia huyu mtoto angalau moja.”
Maombi yangu kwako:
Nairudisha nyota yako uliyoipoteza kupitia wachawi wakati unazaliwa, waganga wa kienyeji kwa kuchanjwa chale, nguo zako ulizopoteza, nywele na kucha ulizokatwa, picha uliyopoteza, sauti yako iliyochukuliwa na kwa njia nyingine yoyote katika Jina la Yesu Kristo aliye hai!
........soma sehemu ya pili ya makala hii kuhusu vitu ambavyo shetani anaibia watu na kuwaacha wakiteseka maisha yao yote.
Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)