Ticker

6/recent/ticker-posts

Nini kinasababisha unabii usitimie?

NINI KINASABABISHA UNABII USITIMIE? JE TUNAHITAJI UNABII LEO? 

Jina nabii (prophet) kwa lugha ya asili ya Biblia limetokana na neno ‘tamka’ na ‘ona.’ Kwa hiyo nabii ni msemaji wa Mungu. Kuhani anapeleka maneno ya wanadamu kwa Mungu na nabii anapeleka maneno ya Mungu kwa wanadamu. Inaaminika kwamba manabii wa Agano la Kale walitumika kama mitume katika Agano Jipya. Kumbuka nilipozungumzia mitume nilisema kuna mitume walioweka msingi wa kanisa (mitume wa Mwanakondoo) na mitume wa kanisa wanaoendeleza ujenzi katika msingi uliowekwa. Watu wengi wanaopinga huduma za mitume hawajui tofauti kati ya mitume walioweka msingi wa Kanisa la dunia nzima (universal) na mitume wanaopanda na kuendeleza makanisa (local churches). Efe 2:20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.

Lakini pia kuna tofauti kati ya HUDUMA YA UNABII  na KARAMA YA KUTABIRI.

Huduma ya unabii ni kati ya huduma tano ambazo zinatolewa na Yesu kwa BAADHI YA WAKRISTO kwa ajili ya kanisa kwa kusudi la:

1. Kukamilisha watakatifu 

2. Kusaidia huduma itendeke na 

3. Kujenga mwili wa Kristo. 

Efe 4:11,12 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe. Hii ni ofisi ambayo mara nyingi haifanyi kazi kwa msimu na inagusa kanisa lote (universal). Ila usije ukachanganya na wale ambao wamepewa huduma hizi na watu au kujipa wenyewe.

Karama ya kutabiri inatolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya MUUMINI YEYOTE kwa kusudi la kuwajenga watu, kuwafariji na kuwatia moyo. 1 Kor 14:3Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Karama hii inaweza kufanya kazi kwa nyakati fulani na kwenye kanisa la mahali fulani tu (local church). Mkristo yeyote anaruhusiwa kutamani (kutaka sana) kuwa na karama hii. 1 Kor 14:1 Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu. Neno ‘kuhutubu’ hapa sio kutoa hotuba au kuhubiri bali ni KUTABIRI (PROPHESYING).

Kwa hiyo manabii wa kweli bado wapo katika kipindi chetu. Pia wanabii wa uongo wapo. Hata katika kipindi cha Biblia kulikuwepo manabii wa kweli na wa uongo. Ndiyo sababu Mungu aliongeza karama ya kupambanua roho ili itusaidie kujua chanzo cha unabii ni Mungu, shetani au roho ya kibinadamu. 1 Wakorintho 12:10 “na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.”

KWA NINI UNABII UNAWEZA KUTOLEWA NA USITIMIE?

1. Chanzo chake sio Mungu bali ni roho ya shetani

Ezekieli 22:28 “Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo Bwana hakusema neno.” Nabii anaweza kutabiri uongo kwa vile ni nabii wa shetani au ni nabii wa Mungu ila siku hiyo amedanganywa na shetani. Ndiyo sababu hatutakiwi kuwahukumu manabii bali tutumie karama ya KUPAMBANUA ROHO. Hata hivyo sio wakristo wote wamepewa karama ya kupambanua roho. Wengi wanaokataa unabii wanatumia saikolojia. Ni hatari sana kutumia saikolojia (akili) katika masuala ya kiroho. 1 Wakorintho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” Shetani anaweza kumtumia nabii wa Mungu kama amefungua mlango kwa shetani. Mfano kama ana uchungu moyoni au hajamsamehe mtu aliyegombana naye, shetani anaweza kumtumia kwa siku hiyo.  Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.”

2. Chanzo chake sio Mungu bali ni roho ya kibinadamu.

Mtu anaweza kutabiri kwa kujikinai mwenyewe. Kumbukumbu la Torati 18:22 “Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope.” Pamoja na kwamba kujikinai au kiburi ni roho ya shetani, hapa nabii ametoa unabii akiwa anajua katika akili yake kwamba anadanganya. Nabii anaweza kutabiri kwa akili zake kwa sababu mbalimbali. Kwanza, inawezekana alikuwa anatumiwa na Mungu akanyang’anywa hicho kipawa na hataki watu wamuone kwamba hatumiwi tena na Mungu. Pili, inawezekana sio nabii bali anatumiwa kwa vipindi tu ambavyo Roho anataka kumtumia lakini yeye anataka aonekane kwamba ni nabii. Tatu, inawezekana kuna watu wanamuendea kama nabii hivyo anataka asiwaangushe. Unadhani mtu atafanyaje kama hana hofu ya Mungu halafu kuna watu wamemjia ili kupata neno kutoka kwa Bwana na anawasikia wakiomba na kusema, Ee Bwana tuko kwa nabii wako mpe neno sasa kwa ajili yetu? Anaweza kuona kwamba itakuwa aibu kama hakusema chochote. Tunapoomba tutarajie kwamba Mungu anaweza kumtumia yeyote na sio mtu fulani maalum. Na tusilazimishe jibu lipatikane siku hiyohiyo.

3. Hatua hazikuchukuliwa kama unabii ulikuwa wa masharti (conditional)

Yona 3:4-5 “Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.” Yona alipotabiri kuhusu kuangamia kwa Ninawi haikumaanisha Mungu anataka waangamie. Mungu alitaka watubu ili wasiangamie. Hata Yona alipoona unabii wake haukutimia kama alivyosema, alikasirika. Yona 4:1,2 “Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika. Akamwomba Bwana, akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya.” Kuna unabii ambao kama hatua fulani zitachukuliwa unaweza kutotimia kama ulivyonenwa. Eze 33:14,15 “Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki; kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang'anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.”

Unabii unaweza kutotimia na bado uwe ni wa Mungu kama ulikuwa unafunua mpango wa shetani na watu wakaomba. Mungu anaweza kufunua kuhusu ajali au mauti itakayotokea mbele. Hatuwezi kusubiri mtu afe ili tuseme unabii ni wa kweli. Kama tutavunja mpango huo kwa maombi jambo hilo halitatokea. Ni mara nyingi Mungu ametoa unabii wa kutahadharisha. 2 Wafalme 6:9,10 “Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili.”

4. Ukaidi na kiburi cha walengwa

Siku moja katika ibada mtumishi wa Mungu alipata unabii kuhusu mtu fulani. Mtu huyo akagoma kutoka mbele. Baada ya ibada ndipo akajitokeza na kusema mtu uliyekuwa unamtabiria ni mimi ila niliogopa kutoka mbele. Hivi unadhani watu ambao hawajui kwamba huyo ndugu alijitokeza baada ya ibada walimtafsiri vipi huyo nabii. Lazima watasema ni nabii wa uongo. Kumbe unabii haukutimia kwa vile mhusika alikuwa mkaidi. Ingawa alijitokeza baadaye hawezi kupokea baraka kamilifu alizokuwa ameandaliwa kwa vile amepishana na wakati muafaka wa Mungu kwake. Mithali 29:1 “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” Pamoja na kwamba Mungu alisema na nabii Yeremia kuhusu kitakachotokea baada ya miaka 70 bado Danieli aliomba na kuungama kwa ajili ya utimilizo wake. Dan 9:2-5 “katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako.”

5. Kutopata tafsiri sahihi

1 Kor 14:29,30 “Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.” Tunawaonea sana manabii kwa kuwatarajia wafanye kazi mpaka ya kupambanua. Kazi ya kupambanua sio ya kwao bali ni ya watu wengine. Kimsingi kupambanua roho kuna kazi kubwa mbili. Kwanza ni kujua chanzo cha ujumbe (umetoka kwa Roho wa Mungu, roho ya shetani au roho ya kibinadamu). Pili, kama unatoka kwa shetani au ubinadamu unakataliwa na kama unatoka kwa Mungu una maana gani. Kama tafsiri sahihi haijulikani unaweza kudhaniwa haukutimia. Wakati mwingine kuna mambo ya kufanya ili unabii utimie. Mfano, mtu anaweza kuona ameketi na Rais wa nchi anampa maelekezo fulani. Kama hana ufahamu wa rohoni anaweza kutafsiri kisiasa kwamba Rais atamteua katika nafasi fulani au anatakiwa agombee nyadhifa za kisiasa.Matokeo yake anagombea nafasi na kushangaa ameikosa. Au anaweza kutafuta nauli akaonane na Rais akidhani ameonyeshwa akakutane naye ikulu. Lakini kimsingi Mungu anaposema nasi anatumia vyeo vya duniani kumuwakilisha. Rais wa nchi anaweza kuwakilisha Mungu (Mfalme wa Wafalme). Kwa hiyo maono hayo yanaweza kumaanisha kwamba mhusika alikuwa anapewa maelekezo na Mungu kuhusu jambo fulani. Tusisahau kwamba nabii anaweza kutumiwa na Mungu kwa sauti (kupewa maneno) au kwa kuona (kupewa maono). Hata hivyo kama ni mwonaji sio lazima alale usingizini ndipo aote na sio lazima afunge macho ndipo aone. Anaweza akiwa anamtazama mtu hapohapo mbele yake apitishiwe picha fulani ambayo wengine hawaioni.

Hata hivyo wakati mwingine nabii hapewi unabii kamili hivyo alitakiwa asiuseme kwanza mpaka pale atakapopata picha kamili. 1 Kor 14:28,32 “Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu. Na roho za manabii huwatii manabii.”

6. Kuzuiwa na shetani

Dan 10:12,13 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.” Hapa tunapata fundisho kubwa sana jinsi shetani anavyoweza kuzuia baraka au majibu yaliyokwisha kuachiliwa mbinguni. Sio malaika wote wanaweza kupambana na falme za shetani hasa malaika wa kuhudumu. Kumbuka aliyemshinda shetani ni YESU KRISTO na sio malaika! Malaika anamwambia Danieli kwamba ilipasa apokee majibu yake siku 21 zilizopita ila amezuiwa angani mpaka alipokuja Mikaeli (malaika wa vita) kumsaidia. Hata Mtume Paulo aliwahi kuwa muwazi kwamba amezuiwa mara mbili na shetani ili watu waombe wasidhani ni ratiba tu imekaa vibaya. 1 Wathesalonike 2:18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.” Tusimfiche shetani pale anapokuwa amehusika kuharibu maisha yetu. Unabii unaweza kusema kwamba fulani atapata wadhifa fulani kanisani au katika serikali na baadaye usitimie. Sababu inaweza kuwa dhambi ya mhusika baada ya unabii au kutovunja madhabahu za shetani zilizokalia kiti hicho siku nyingi. Kama shetani ana agenda fulani na akagundua kwamba ukikaa wewe hutaitekeleza vizuri ataleta upinzani mkali. Lazima maombi ya kimkakati yafanyike. Watu wengi wamecheleweshewa majibu yao mpaka wamehalalisha kwamba sio mpango wa Mungu. Ukuta wa Yeriko ulihitaji siku 7 kuuangusha. Unadhani wangechoka na kuishia siku ya tano ingekuwaje?  Maombi hafifu hayawezi kuruhusu upate ahadi zako kutoka kwa Bwana hata kama aliahidiwa mbele ya mashahidi wengi. Pambana kwa Jina la Yesu mpaka kieleweke!

7. Bado wakati wake haujafika

2 Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.” Sio kila unabii utatimia mapema kama tunavyofikiri. Mfalme Daudi alitiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli akiwa na takriban miaka 17 lakini unabii huu ulitimia baada ya miaka 20. Na katika kipindi chote hicho alipitia nyadhifa mbalimbali ili apate uzoefu kv kumpigia mfalme kinubi, kusimamia jeshi na kuongoza Hebroni ndipo akatafutwa kutawala Israeli. Ni vigumu sana mtu kuwa Rais wa nchi hata kama Mungu alisema naye kama hataanza kutumika katika nafasi za chini ili apate uzoefu na kufahamika uwezo wake. 1 Petro 1:12 “Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.” Kuna unabii mwingine utatimia kwa watoto wako au kwa wajukuu zako. Kuna unabii katika Biblia ambao bado haujatimia. Mfano,kurudi kwa Bwana Yesu nk. Mt 24:29-30 “Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.”

Angalizo:

1. Kutimia kwa unabii au ukweli wa unabii peke yake havitoshi kuthibitisha kwamba unabii ni wa Mungu

Tuangalie unabii unatuelekeza kumwabudu nani. Kum 13:1-4 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.” Hupaswi kumkubali nabii ambaye ana ushuhuda mbaya ambao umethibitika hata kama anachokuambia ni kweli. Wapo manabii leo ambao wanatukuza majina yao kuliko Jina la Yesu ambalo tumetumwa kuliinua.

Hata pepo wa uaguzi anaweza kusema ukweli ili aaminike ndipo baadaye apotoshe. Mdo 16:17 “Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.”

2. Tumeonywa tusiudharau unabii bali tuupime na kuchukua la kweli na kuacha la uongo.

1 The 5:20-22 “msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna.” Sio lazima nabii akisema ukweli leo na kesho aseme ukweli na sio lazima nabii akisema uongo leo na kesho aseme uongo. Kazi yetu ni kupima kila wakati na kuepuka kuwa na chuki binafsi na nabii au kumuamini nabii kupita kiasi. Ukimchukia nabii utatafuta tu makosa na kamwe hutaona zuri. Ukimuamini sana kwamba hakosei unaweza kupotea kama ataingiliwa na shetani. Ni Mungu peke yake ambaye hawezi kukosea (infallible).

MADHARA YA KUKOSA UNABII WA MUNGU 

1. Unaweza kujiona uko shwari kimwili kumbe una hali mbaya.

Mithali 14:4 “Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.” Andiko hili lina maana kwamba kama mtu hafugi ng’ombe zizi lake litakuwa safi. Akifuga ng’ombe uchafu utakuwepo lakini atapata maziwa. Sasa uchague: Kanisani pasiwepo unabii ili tusije tukadanganywa au unabii uwepo halafu uongo tuukatae na lakini tujue ukweli wa Mungu kuhusu maisha yetu. Kanisa linaweza kudhani liko shwari kumbe kuna wezi wengi ambao wanaliibia na haiwezekani kuwagundua kama roho ya unabii haitakuwepo. Yapo makanisa yanayokejeli watumishi wanaokemea mapepo kwa watu. Siku moja mtu fulani akaniambia hivi ninyi mbona makanisa yenu yana mapepo sana? Nikamwambia kama hakuna nguvu ya Mungu watu watalogana kimyakimya na mtadhani mko salama. Niliwahi kukaribishwa kanisa moja kuhubiri. Nilipoombea watu, mtu aliyekuwa anategemewa sana akaanza mapambano na mwingine sababu ya uchawi. Watu waliachwa midomo wazi maana walikuwa wanasikia tetesi lakini walikuwa hawaamini vizuri. Watu wanaweza kujiona wako shwari lakini ukiwafuatilia sana wana magonjwa mazito, wanakabwa na majinamizi, wanabakwa kwenye ndoto, wanaamka wamechoka kwa vile wanalimishwa usiku kiroho, hawapatani, wanadhulumiana, hawana upenyo wowote maishani hata wakijibidisha na kazi, wanaanguka na kujutia kila mara, ndoto za maisha yao zimevurugika, wana roho za kukataliwa nk. Hizi zote ni tabia za mapepo hata kama mtu anajitahidi vipi kuimba kwaya na kutumika kanisani.

2. Kanisa haliwezi kuwa na afya kamili

Ikiwa Bwana Yesu amesema ametoa huduma tano ili kukamilisha watakatifu kwa ajili ya kutumika vizuri na kanisa kujengwa, hatuwezi kudharau baadhi ya huduma zake halafu tuwe salama. Efe 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.” Kila huduma ina jukumu lake katika mwili wa Kristo hakuna ambayo ni ya muhimu kuliko nyingine ingawa ipo inayoweza kutangulia ndipo ifuate nyingine.

3. Kutumika kwa kubahatisha

Matendo ya Mitume 21:11 “Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.” Kama hakuna unabii unashtukizwa na matatizo na majaribu mbalimbali. Na kama utashtukizwa na matatizo ni rahisi kukuzidi nguvu maana hujajiandaa. Ni vizuri kujua mipango ya adui iliyoko mbele ili uikemee na mipango uliyopangiwa na Mungu ili uidai vizuri. Lakini pia unaweza kujikuta unatumika katika huduma unayoipenda na kuacha ile uliyopewa na Mungu. Hali hii itasababisha usipate upenyo na matokeo mazuri maana malaika wametumwa kwingine na wewe umeenda mahali pengine tofauti. Kwa lugha nyepesi unakuwa umepishana na Mungu. Hakuna maana kupata sifa duniani wakati mbingu haina taarifa za huduma yako. Huwezi kulipwa siku ya mwisho. 

4. Kudanganyika kwa wepesi

Mathayo 24:11 “Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.” Katika kipindi cha Biblia walitahadharishwa kuhusu unabii wa uongo kwa vile walikuwa tayari wanajua unabii wa kweli. Leo kuna watu wamekazana tu kuwaita wenzao manabii wa uongo lakini ukiwauliza unabii wa kweli ni upi hawana jibu. Sababu kubwa ya waumini wengi kutumbukia kwa manabii wa uongo ni kwa sababu katika makanisa yao tangu wajiunge hawajawahi kusikia unabii na wana mahitaji yanayohitaji huduma ya nabii. Wangejua unabii wa kweli wangeweza kupima kwa wepesi. Matokeo yake wanawaendea watu ambao hawana UNABII WA MUNGU bali wana PEPO LA UAGUZI. Pepo la uaguzi linaweza kusema kitu cha kweli kabisa. Mdo 16:16-18 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” Hili pepo la uaguzi lilisema ukweli kuhusu mtume Paulo. Ila Paulo akakasirika moyoni ingawa ujumbe ni wa kweli. Akagundua chanzo sio sahihi. Alipokemea kwa Jina la Yesu, pepo likamtoka huyo mtu. Wapo manabii ambao wanatumika kama walivyo waganga wa kienyeji na wapiga ramli kwa vile unabii wao sio wa Mungu. Mganga wa kienyeji anaweza kukuambia ukweli wa jambo lililokupata na hata kujua majirani zako ni kina nani. Sio lazima mtu akikubashiria jina la mama yako na anakotoka awe ni nabii wa Mungu. Kazi kubwa ya unabii ni kukujulisha mapenzi ya Mungu. Na kamwe Mungu hatakufanyia kila kitu bila wewe kuhusika. Usidanganyike kwamba utabarikiwa kwa kutoa sadaka sh 10,000 na kisha kusema, “Pesa njoo!” Utajiri wa ki-Mungu una kanuni zake.

Wewe unayehitaji msaada wa Mungu omba sala hii kwa imani:

Ee Mungu wangu najua umeniweka hapa duniani kwa kusudi maalum. Nijalie kutambua thamani yangu. Badilisha maisha yangu unifanye vile unavyotaka niwe. Niongoze nitambue mipaka yangu. Nisihukumu nisije nikahukumiwa. Nipe macho ya kuwatambua watumishi wa kweli na wa uongo ili niishi katika mapenzi yako siku zote za maisha yangu. Ninaomba haya katika Jina la Yesu Kristo. Amina.

Dkt. Lawi Mshana, +255712924234; Tanzania

Post a Comment

0 Comments