Ticker

6/recent/ticker-posts

Mambo yanayotufanya tushindwe kuwasaidia watu kama Mungu anavyotaka

MAMBO YANAYOTUFANYA TUSHINDWE KUWASAIDIA WATU KAMA MUNGU ANAVYOTAKA – Lawi Mshana

Mara nyingi tumekuwa kikwazo kwa watu kumuona Mungu kwa kumuwekea Mungu mpaka katika utendaji wake. Wakati mwingine utasikia mtu hata asiyejua sauti ya Mungu wala kuijua Biblia vizuri anasema, ‘Mungu hawezi kufanya hivi!’ Kuna wakati mtu anaweza kuwa sahihi kwa kusema hivyo lakini wakati mwingine ni kutojua utendaji wa Mungu tofauti na aliouzoea. Hata kipindi cha Biblia watu walimpa mpaka Mungu. Zaburi 78:41 ‘Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli’.

Leo mchana wakati naomba Roho alinipa mambo kadhaa yanayotufanya tushindwe kumuona Mungu akijidhihirisha inavyotakiwa.

Zifuatazo ni kasoro ambazo ni kikwazo katika utumishi wetu.

1. SIKUOMBEI UPONYAJI MPAKA UOKOKE KWANZA.

Kuna watu hawajui kwamba Mungu hana formula maalum katika utendaji wake. Mtu mmoja anaweza kuokoka ndipo aponywe wakati mwingine anaponywa ndipo aamue kuokoka. Watu wengi walioponywa na Bwana Yesu hakuna ushahidi kama walimpokea kwanza kama Bwana na Mwokozi wao. Waliamini tu kwamba anao uwezo wa kuwaponya magonjwa na misiba yao. La msingi mtu awe na hitaji la kuponywa na Bwana. Luka 9:11 ‘Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa’. Hata hivyo mtu aliyeponywa kama hataokoka uponyaji wake unaweza usiwe wa kudumu. Lakini kutookoka kwake hakumzuii Mungu kumponya.

2. USIPOABUDIA KWETU HUTAPOKEA MUUJIZA

Kuna wakristo wanadhani wao wana “haki miliki” ya miujiza ya Mungu. Hata wanafunzi wa Yesu waliwahi kuwa na mawazo kama haya ikabidi Bwana awasaishea. Mk 9:38,39  ‘Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya.’ Watu wa aina hii hawako tayari kutambua muujiza uliofanyika kupitia kanisa jingine. Wanataka Yesu wa miujiza awe wa kwao tu. Na wanataka kila muujiza unapofanyika uongeze watu kanisani kwako tu na sio katika ufalme wa Mungu. Yesu ana mazizi mengi. Yn 10:16 ‘Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.’

3. HUWEZI KUOKOKA MPAKA UONGOZWE SALA YA TOBA

Sala ya toba imekuwa kama utamaduni wa kanisa. Tunasahau kwamba kuna tofauti ya KUTUBU na KUONGOZWA SALA YA TOBA. Biblia imetaja zaidi neno TUBUNI bila kueleza namna watu walivyotubu. Walichozingatia zaidi ni matendo baada ya mtu kusema ametubu. Mdo 26:20 ‘bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao’. Yesu aliwahi kutambua toba ya mwanamke bila kumuongoza sala ya toba. Yesu aliangalia matendo yanayodhihirisha toba yake. Lk 7:47 ‘Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.’ Mtu anaweza kutubu kwa maneno yake mwenyewe au hata kwa kutumia Zab 51. La msingi ajisikie kwamba amemtenda Mungu dhambi na amgeukie Yesu kama sadaka ya Mungu kwa ulimwengu. Wapo pia ambao wamewahi kutubishwa na Yesu katika maono. Lakini pia tuna watu walioamua kuongozwa sala ya toba ili WAMUOKOKEE fulani akubali kuwa mchumba wake.

4. UKIMPOKEA YESU TAYARI UMEJAZWA ROHO MTAKATIFU

Kuna watu wanasema ukishampokea Yesu hakuna haja ya kuombewa ujazo wa Roho Mtakatifu. Matokeo yake tuna watu wameokoka lakini ni wakavu sana katika masuala ya kiroho. Mdo 19:2,6 ‘akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.’ Si makanisa mengi yanaombea watu ujazo wa Roho Mtakatifu mara kwa mara. Ipo lugha ya Roho na ya mazoea. Wengine wananena lugha ya maneno hayohayo kwa kila kitu wanachoombea. Utashangaa mtu akiombea mchungaji, kanisa na yeye mwenyewe anasema maneno hayohayo – rikababasai. Hii inatia mashaka kwamba hafanywi upya kila wakati. Ujazo wa Roho sio suala la mara moja kwa vile mafuta yanatumika mara kwa mara tunapopanda milima ya majaribu.

5. UKIMPOKEA YESU HAKUNA HAJA YA UKOMBOZI (KUFUNGULIWA)

Ni ukweli usiopingika kwamba tuna watu waliookoka lakini bado wanaanguka dhambini kama walivyo wapagani. Hakuna kanisa ambalo halina watu wanaoanguka dhambini. Rum 12:2 ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.’ Mtu anaweza kuokoka lakini bado anaishi kidunia na hajafanywa upya. Isa 61:1 ‘Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.’ Tuna watu wengi ambao wameokoka lakini bado wana vifungo vingi vya umasikini, magonjwa, mahusiano, madeni nk. Au je hakuna maandiko ambayo bado hatujaweza kuyatekeleza ingawa tumeokoka? Mfano, Kum 15:6 ‘Kwani Bwana, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.’

6. DHEHEBU LETU NDILO PEKEE LIMETOKA KWA MUNGU

Kwanza lazima tutambue kwamba mbinguni hakuna kitabu cha madhehebu bali kuna kitabu cha uzima chenye majina ya watu waliomwamini Bwana Yesu. Madhehebu yanatusaidia tu duniani kutambulika uhalali wetu katika serikali. Ukifuatilia hata katiba za madhehebu mengi utagundua kwamba wanayofanya ni tofauti na misingi ya imani waliyoiandika. Wakati mwingine dhehebu linaweza kuwa na misingi ya imani yenye utata lakini hutakosa watu ambao wana imani ya kweli. Lakini pia unaweza kusoma misingi mizuri ya imani ya dhehebu fulani wakati baadhi ya watu wake wamemuacha Mungu siku nyingi. Tusihukumu watu kwa madhehebu yao Mungu ndiye anajua kina nani ni watu wake. 2 Tim 2:19 ‘Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake.  Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.’

7. LAZIMA UTOE KITU NDIPO UOMBEWE

Sio mpango wa Mungu huduma za maombezi zifanywe kitega uchumi. Pia Mungu hapendi watu walipie huduma alizozitoa bure. Mathayo 10:8 ‘Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.’ Hata mtume Paulo alisema hapendi kuwalemea watu kwa huduma yake ikabidi ashone mahema ili kujiingizia kipato. 2 Kor 12:13 ‘Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe udhalimu huu.’ Hata Bwana Yesu hakulemea watu. Kwa hiari yao watu waliamua kumhudumia kwa mali zao kwa vile wamewekwa huru. Lk 8:2,3 ‘na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.’ Kama mtumishi hatakuwa na njia halali za kumuingizia kipato au Mungu kumuinulia watu wa kumtegemeza lazima atalazimika kuitumia huduma ya kiroho kama mradi wake.

Wapendwa Mungu atusaidie ili tuwafikie watu bila ubaguzi kama Mungu wetu anavyowapa mvua wema na wabaya. Mt 5:45 ‘ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.’

 

Post a Comment

0 Comments