Ticker

6/recent/ticker-posts

KWANINI WAUMINI WENGI HAWAFANIKIWI KIUCHUMI


KWANINI WAUMINI WENGI HAWAFANIKIWI KIUCHUMI? 

Zipo sababu nyingi za waumini kutofanikiwi kiuchumi ingawa wanaonekana kama wako vizuri kitabia. Ngoja nikupe sababu kadhaa kati ya nyingi zinazosababisha ugumu huo. 

1. Kwa sababu wanaishi kwa ajili yao wenyewe na hawamtangulizi na kumtii Mungu maishani kama wanavyopaswa Kipindi cha nabii Hagai waumini walikimbilia kujenga nyumba zao za kifahari na kusahau kumjengea Mungu. Kilichotokea ni kupata mavuno kidogo, kutotosheka, kutonufaika na kipato chao na mishahara yao kutofanya cha maana. Hag 1:1-11 “…Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu…..” Isa 1:19-20 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.” Unaweza kuwa muumini mzuri unayefaa kwenda mbinguni na ujikute hapa duniani unaishi maisha magumu badala ya KULA MEMA YA NCHI. 

2. Kwa sababu wanatumainia mfumo wa uchumi wa dunia na uwezo wao wenyewe au fedha zao badala ya Mungu. Kipindi hiki uchumi wa dunia umetikiswa. Hivyo wataaibika wengi wanaotumainia uchumi wa dunia badala ya kumtegemea Mungu atupaye vitu vyote. I Tim 6:17 “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.” Wakati dunia inajivunia mali za dunia hii sisi tunapaswa kujivunia Mungu wetu aliye hai. Mungu ana njia nyingi za kutubariki maana yeye hafi, hafilisiki na wala hawezi kubadili nia yake. Zab 20:7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.” 

3. Kwa sababu wanatembea katika hofu ya kupungukiwa (fear of lack). Ayubu anasema kwamba jambo lile unaloliogopa ndilo litakalokupata. Ayu 3:25 “Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia.” Sisi sio watu wa kujisumbua bali tunapaswa kuweka tegemeo letu kwa Mungu wetu ambaye kamwe hatatuacha tuaibike. Fil 4:6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Lk 12:32 “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.” 

4. Kwa sababu hawatoi zaka. Zaka ni sheria ya kiroho iliyoko kwenye Neno la Mungu. Kama unamheshimu Mungu kwa kuimba kwaya, tenzi na mapambio peke yake sahau kupata mafanikio ya kiuchumi. Lazima umheshimu Mungu kwa mali zako pia na ndipo pochi yako, stoo yako na akaunti zako zitajaa baraka. Mit 3:9-10 “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.” Zaka ni ya muhimu sana kwa serikali ya Mungu ila isikufanye upuuzie mambo mengine ya msingi. Usijisifu kwa kutoa zaka wakati unaishi maisha ya dhambi. Mt 23:23 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.” Kuna watu wanasema zaka haijatajwa kwenye Agano Jipya ili wahalalishe kutokutoa kwao. Lakini watu hao hao wanatumia baadhi ya maandiko ya Agano la Kale kwa ajili ya kuomba mafanikio kv Mimi ni kichwa wala si mkia. Ila wakifikia kwenye kutoa zaka wanalikataa Agano la Kale. Zaka imerudiwa kwenye Agano Jipya kwamba wanadamu wanaokufa hutwaa zaka (sehemu ya kumi). Ebr 7:8,9 “Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi” 

5. Kwa sababu baada ya kutoa zaka, hawatoi sadaka kwa ukarimu, kwa hiari na kwa ukunjufu. Mungu hapendi mtu amtolee wakati ana kinyongo, amenuna au amejilazimisha. Kwa kawaida Mungu anaangalia MOYO kabla ya MKONO wako wakati unapomtolea sadaka. Tunatakiwa tuone kwamba utoaji ni fursa na sio hitaji au tatizo. 2 Kor 8:1-4 “…..Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.” Unapokuwa bahili au mchoyo kwa Mungu utajikuta unaishiwa mara kwa mara kuliko yule anayetoa kwa ukarimu. Kumbuka ni Mungu anayekufanya ubaki na pesa kwa kukuepusha na magonjwa, mikosi na ajali nyingi. Mit 11:24-25 “Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.” 2 Wakorintho 9:7 “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” 

6. Kwa sababu hawatoi zaka na sadaka kwa imani. Ebr 11:33 “ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba”. Usitoe zaka kama wajibu wa kidini bali kwa kuonyesha upendo wako kwa Mungu na kumtambua kama chanzo chako cha mafanikio. Toa kwa imani ukitarajia Mungu kukubariki kama alivyoahidi. Toa zaka na sadaka KWA FURAHA. Toa zaka na sadaka KWA IMANI. Formula ya mafanikio ya kiuchumi: Mpe Mungu 100% ya moyo wako na 10% ya mapato yako (pamoja na matoleo ya ukarimu). 

7. Kwa sababu sio waaminifu na hawana bidii (diligent). Kuna watu wanajitahidi kutoa lakini wana tabia ya kudhulumu na kutapeli watu. Wanatumia kanisa kama kichaka cha kujificha kwa njia ya utoaji wao. Matokeo yake baada ya muda wanaadhibiwa. Mit 28:20 “Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.” Mit 11:1 “Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.”; Mit 20:23 “Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa Bwana; Tena mizani ya hila si njema.” Wengine ni wavivu na hawajali kuweka akiba wala kuwekeza. Biblia inasema watu hawa wanashindwa na wadudu kama sisimizi wanaoweka akiba. Mit 10:4 “Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.”; Mit 6:6-11 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.” 

8. Kwa sababu hawana maadili ya Kibiblia ya kazi. Kuna watu hawana heshima kwa wakuu wao kwa kisingizio kwamba wanamheshimu Mungu peke yake. Lakini pia kuna mabosi wanajitahidi kumtolea Mungu lakini wanawadhulumu watumishi wao. Wengine ni viongozi wa kanisa lakini hawataki kuwalipa posho wasichana wao wa kazi za nyumbani. Efe 6:5-9 “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo; wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo; kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu; mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru. Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.” Lazima tuwajibike kwenye kazi za watu kama vile tunamtumikia Mungu. Vinginevyo hatuna haki ya kudai kulipwa posho au mshahara. Kol 3:22-24 “Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.” 

9. Kwa sababu hawawaheshimu (hawawasaidii kifedha) walio katika huduma. Kama watumishi wa Mungu wanatumika kwa kujigharamia wenyewe tusitegemee kupata baraka za kudumu. Ni wajibu wa waumini kuwahudumia watumishi wanaowapa malezi ya kiroho. I Kor 9:7-14 “Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi? Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo? Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.” Wengi wamezoea kushirikisha matatizo tu kwa watumishi wa Mungu lakini hawawashirikishi baraka zao. Neno linatuagiza kwamba tuwashirikishe wakufunzi wetu baraka tunazozipata. Gal 6:6 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.” Tambua uhusiano wa heshimu na msaada wa kifedha: Mit 3:9 “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.”; Mit 14:31 “Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.”; I Tim 5:3 “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.” Kenneth E. Hagin: Katika kitabu chake cha Kuheshimu Mchungaji wako—anasema kwamba wote wanaoheshimu Mchungaji wao watafanikiwa katika maisha. 

10. Kwa sababu hawatumii hekima katika fedha zao. Pamoja na kuongeza kipato lazima kuwa na hekima katika matumizi ya baraka tunazopata. Mit 3:13-18 “Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.” Mit 11:29 “Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.” Mit 21:20 “Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.” Hii ni sawa na kusema, “Nyumba ya mwenye hekima imejaa vitu vya thamani lakini mtu mpumbavu anatapanya mali zake.” Jihadhari na mikakati ya aina yoyote ya “kupata utajiri kwa haraka”

Unaweza ku-share ujumbe huu kwa wengine na kutoa maoni yako. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania

Post a Comment

0 Comments