KWA NINI
WATUMISHI MATAPELI WANAONGEZEKA KWA KASI KIPINDI HIKI? – Dr Lawi Mshana
Kumekuwa na
ongezeko la waumini kutapeliwa na watu wanaojiita watumishi wa Mungu. Baadhi ya
sababu za kutapeliwa zinatokana na watumishi hao na zingine zinatokana na
waumini wenyewe.
Napenda kukupa
sababu kadhaa nilizojaliwa kuzijua ili uchukue tahadhari au hatua:
1. Ilitabiriwa
katika Maandiko Matakatifu kwamba watatokeo watumishi matapeli
Mt 24:24,25 “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.” Maneno haya yanatoka kwenye kinywa cha Bwana Yesu mwenyewe. Bado tuko katika hatua za awali sana za udanganyifu utakaoletwa na shetani kwa kutumia watu wanaojiita watumishi wa Mungu. Kwa vile shetani anajua sio wote watakaowaendea waganga wa kienyeji, ameandaa watu wanaojiita watumishi au manabii ili waaminike kirahisi. Amewapa uwezo wa kutoa ishara na maajabu ili ikiwezekana (kama yamkini) HATA WATEULE WAPOTEE. Itafika wakati watafanya moto ushuke kutoka mbinguni ili tu kuwadanganya watu wasioijua kweli ya Mungu. Ufunuo wa Yohana 13:13,14 “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.”
2. Dhana kwamba mtumishi akifanya kazi za kipato, upako wake utapungua
Mtume Paulo ni kati ya watumishi wa Mungu waliotumiwa sana na Mungu lakini alifanya kazi ili asiwalemee watu. 1 Wathesalonike 2:9 “Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.” 2 Wakorintho 12:16 “Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa hila.” Ni kweli watu wanatakiwa kumtolea Mungu sadaka lakini isifike mahali wakalazimishwa kutoa zaidi ya uwezo wao na zaidi ya mpango wa Mungu. Kuna watumishi wanadhani kwamba kama watafanya kazi za mikono upako wao wa kuombea na kuhubiri utapungua. Ila ukifuatilia sana hawaombi masaa yote bali kuna masaa wanaangalia tamthilia, wanachati, wanapiga soga, wamekaa tu au wamelala tu tena mchana kweupe. Unapokuwa hufanyi kazi za kuingiza kipato lazima utalazimika kuwafanya unaowapa huduma za kiroho wawe mtaji kwa vile hata sehemu unayofanyia maombi hutaweza kuilipia na wala hutaweza kusomesha watoto. Ikifikia mahali ukatingwa na majukumu ya kuhudumia watu, Mungu atakuinulia watu wa kugharamia huduma lakini sio kulipisha kila anayehudumiwa. Hata Bwana Yesu alikuwa na watu wenye upako na huduma ya kumhudumia kwa mali zao. Hii ilimfanya asihitaji michango kwa kila mfuasi wake. Lk 8:1-3 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.” Tangu nianze huduma miaka zaidi ya 20 iliyopita sijapiga simu kuomba muumini anirushie vocha wala kuomba misaada binafsi katika kanisa ninalochunga na makanisa ninayotembelea kwa semina. Kwa kufanya hivyo Mungu amekuwa mwaminifu kwangu kwa kubariki kazi za mikono yangu na kuniinulia watu ambao kwa hiari yao wanachangia huduma niliyopewa.
3. Kuingia
katika utumishi kabla ya kufunguliwa au kukombolewa
Kuna mchakato ambao mtu anapitia hadi kutumika vizuri katika huduma aliyopewa. Mitume wa Bwana Yesu walihitaji muda wa KUKAA NAYE wa kutosha ndipo baadaye wakapewa mamlaka. Mk 3:14,15 “Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.” Usidhani kwamba walipewa amri siku hiyohiyo alipowaita. Alikaa nao kwa muda ndipo siku moja akawaita na kuwapa uwezo na mamlaka. Luka 9:1 “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.” Kuna watu wakati wanampokea Yesu walikuwa na mapepo au vifungo mbalimbali na wakaanza huduma bila kuombewa kwanza ili wawe huru. Matokeo yake bado tabia za asili na za kishetani zimewatawala. Wengine wameingia katika utumishi na roho zilizowatawala kwa miaka mingi za wizi, uzinzi, uongo, umasikini, uchawi nk. Matokeo yake ujanja uleule walioutumia wakiwa duniani wanauingiza kanisani. Nimewahi kuombea watumishi kadhaa nikaona mapepo yakijidhihirisha na kuwatoka. Ilikuwa rahisi watumishi hao kufunguliwa kwa vile waumini wao hawakuwepo na hawakuficha ugonjwa. Watumishi wengi wamekwama maisha ingawa wanawaombea wengine kwa vile wana vifungo ambavyo wanaona aibu kuvisema ili wafunguliwe. Usiridhike kufanya huduma ya kuombea na kushauri watu wakati unajisikia kuwatamani? Pona kwanza usije ukahubiri wengine na mwisho wewe mwenyewe ukataliwe. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
4. Kuingia katika utumishi kwa lengo la kuongeza kipato badala ya kuokoa roho za watu
Mungu anataka tuwatoe watu kwenye mateso na kuwaingiza katika ufalme wake. Yuda 1:23 “na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.” Matendo ya Mitume 26:18 “uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Si mpango wa Mungu kuendelea kuongeza waumini ili sadaka ziongezeke wakati waumini hao wanatembea na misiba yao. Badala ya kusema nina waumini kadhaa tunatakiwa kujiuliza wangapi kati yao wako huru na hawatumikishwi tena na shetani. Bado tumejaza watu wenye matatizo makubwa ya kiroho, kimwili na kimaisha na hakuna mkakati wowote wa kuwanyakua katika moto zaidi ya kuhitaji michango yao tu. Siko kinyume na utoaji kwa vile ni agizo la Mungu. Lakini Mungu huyohuyo ameagiza kwamba tufufue wafu, tupoze wagonjwa, tutakase wenye ukoma na tutoe pepo BURE BILA KULIPISHA WATU KWA VILE HATUKUNUNUA HUDUMA HIZO. Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.” Wapo watu ambao wameingia katika utumishi kwa ajili ya kipato na sio kutumika. Watumishi wa aina hii wanathamini fedha kuliko roho za watu. Hata kama huendi kanisani kama unatuma michango ya kifedha wanakuona ni mshirika/msharika hai. Pia hawajali waumini wa kipato cha chini kwa vile hawana cha kutoa. Hata hivyo wapo waumini ambao ni masikini kwa kujitakia kwa vile hawataki kufanyia kazi Neno la Mungu.
5. Kuzama katika ulimwengu wa roho bila ufahamu wa kutosha
Kuna watumishi wanaenda milimani na kufunga na kuomba bila ufahamu wa kutosha kuhusu tofauti ya sauti ya Mungu na sauti ya shetani. 2 Timotheo 3:13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.” 1 Wakorintho 2:13,14 “Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” Mtu anapokuwa haelewi vizuri ulimwengu wa roho halafu akaingia huko kichwakichwa anaweza kuamini uongo wa shetani akidhani ni Mungu amesema naye. Mbaya zaidi ni pale mtu anapofanya maombi haya kwenye mlima wenye maagano ya kishetani na unaotumiwa na wachawi. Wapo watumishi wanaodhani wana karama ya unabii na kumbe ni pepo la uaguzi ambalo linajua maisha ya watu kama wapiga ramli na wachawi. Waumini wengi wanapenda kumsikia mtu anayewaambia kuhusu maisha yao hata kwa mambo ambayo wao wenyewe wanayajua. Hivi inasaidia nini mtumishi akikuambia umevaa sidiria nyekundu hata kama umeivaa kweli. Ipo sababu ya maana ya kuitikia kwa kusema, SEMA BABA, CHIMBUA BABA! Tupende zaidi kumsikia Mungu akisema nasi masuala ya msingi ya kusudi lake na hatima yetu.
6. Kutumika chini ya dhehebu ambalo limeanzishwa na shetani
Kwa vile shetani amegundua ujinga wa waumini wengi, ameanzisha madhehebu yake yenye majina ya kikristo. Ukiwa nje utadhani Bwana Yesu ametawala ila ukiingia na kukaa kwa muda ndipo utagundua mambo yako tofauti kabisa. 1 Tim 4:1-3 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.” Unaweza kuwa muumini mzuri kwenye dini fulani lakini umeshajitenga na imani (umeshamkana Yesu). Shetani anapoanzisha kanisa lake anahakikisha madhabahu yake ameichimbia sadaka zake. Ukisimama kwenye madhabahu hiyo hutaweza kuhubiri kinyume nayo maana uvuvio uliopo ni wa shetani. Kama mtumishi alijiunga bila kujua kama atakuwa kinyume anaweza kufa ghafla kwa vile amekula kiapo. Labda aombewe na mtumishi anayejua jinsi ya kuvunja maagano hayo. Na kama mtumishi ataweza kutoka katika dhehebu hilo kama hataombewa vizuri anaweza kufilisika au kuwa kama zezeta. Lakini sio dhehebu peke yake bali hata kanisa linaloongozwa na mtumishi aliyejisajili kwa shetani. Ndiyo maana sio busara kwa nyakati hizi ukiwa safarini kuuliza kanisa lenu. Sio lazima mchungaji wa kanisa jingine awe kama wa kwako hata kama wanatumika katika dhehebu hilohilo moja.
7. Mtumishi aliyekusudiwa kutumika chini ya baba kuamua kuwa baba yeye mwenyewe
Hata katika hali ya kawaida sio kila mtu anaweza kuwa baba hata kama anataka. Mtoto wa miaka 10 anaweza kuwa na upeo mkubwa lakini hawezi kuwa baba. Vivyo hivyo mtumishi asipokuwa mwangalifu anaweza kuwa baba kabla ya wakati wake na kuhatarisha maisha yake. Hii ndiyo sababu mtumishi mwingine anajikuta akiwa na wakati mgumu sana anapoamua kutumika bila baba wa kiroho na kihuduma. Kinachotokea ni kuanza kutumia ujanja ili huduma hiyo iende. Mtumishi fulani aliwahi kunishirikisha kisa hiki. Aliniambia alishiriki kongamano la kiroho na siku ya mwisho akashangaa mtumishi wa kanisa hilo akisema Roho amemwambia kila mtu atoe alicho nacho ili abarikiwe. Mwisho wa kongamano akamuuliza kwa nini alifanya vile. Akamwambia, ‘Wewe unadhani tungeponaje pale? Niliona pesa za kulipia ukumbi hazitoshi.’ Bilashaka washiriki walikuja wachache kuliko matarajio yake na sadaka walizotoa zikawa chache. Tujifunze kupambanua roho. Wafilipi 2:22 “Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake.” Lazima mtumishi atambue safari ya huduma yake. Asidhani utumishi ni bango la kanisa au wadhifa (cheo au jina) au usajili serikalini. Lazima mtumishi ahakikishe kuna mafuta (upako) yanayomshukia kutoka juu ili apate upenyo kamili wa huduma yake. Zab 133:1-3 “1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.”
8. Waumini wengi kutaka mafanikio kwa njia za mkato
Wapo waumini wanadhani kazi za mokono ni laana. Wanasahau kwamba hata kabla ya uasi Mungu alimuweka Adamu kwenye bustani ya Edeni ili aitunze na kuilima. Mwanzo 2:15 “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” Kwa hiyo wapo waumini wanataka kupata pesa kwa kutabiriwa tu bila kufanya kazi yoyote. Lazima tutambue kanuni za Mungu za mafanikio. Mungu hawapi watu wake utajiri bali anawapa NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI. Kumbukumbu la Torati 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Kama Bwana Yesu hangezingatia kanuni ya Mungu kuhusu jinsi atakavyokuwa mfalme angekubali watu wamfanye mfalme. Yn 6:14,15 “Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.” Bwana Yesu alijua kwamba hakuna njia ya mkato ya kuwa mfalme bali ni kwa kupitia msalabani tu. Unabii peke yake hauwezi kusababisha kusudi la Mungu juu ya maisha ya mtu libadilike.
9. Waumini wengi kuwa na imani tegemezi badala ya kujisimamia
Waumini wengi wanategemea kuombewa bila wao wenyewe kufanya lolote zaidi ya kusema ‘NAPOKEA!’ Muumini anatoka nyumbani anaenda kuombewa na mtumishi ambaye hamjui vizuri na bado haombi Roho wa Mungu amuongoze. Matokeo yake badala ya kupokea Roho wa Mungu anapokea roho nyingine au roho zidanganyazo. Ezekieli 2:1 “Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.” Hata kama mtumishi wa Mungu atakuombea huwezi kupokea kwa ukamilifu kama hutaendelea kuomba. Mtumishi anaweza kusababisha malaika atumwe kwako akiwa na jibu lako lakini ashindwe kukufikishia kama hutatengeneza mazingira ya kupokea. Shetani anaweza kuteka baraka zako zikiwa zimefika karibu sana na wewe kama hukuomba vizuri. Dan 10:12,13 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.” Ufalme wa Uajemi ulizuia majibu ya Danieli kwa siku 21. Sijui falme za giza za kwenu zimezuia majibu yako kwa miezi au miaka mingapi.
10. Kukosa uvumilivu na subira
Mungu hachelewi wala hawahi. Hivyo kama tunataka kuwa salama tunahitaji kuwa na uvumilivu na subira. Luka 21:19 “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.” Yakobo 5:11 “Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.” Wacha Mungu waliotutangulia walikuwa na subira. Wengine leo wamefanya uchaguzi mbaya kwa kushindwa kusubiri. Wapo ambao walioa na kuolewa kabla ya wakati wa Mungu matokeo yake wakaangukia pabaya. Mungu anapofunga mlango usijaribu kuuvunja bali subiri akuonyeshe ni mlango upi uko wazi kwa ajili yako. Kwa vile hatutaki kujihoji na kujiandaa kwa ajili ya baraka tulizoahidiwa na Mungu tunawatafuta manabii watuambie tunachokitaka. Matokeo yake tunapewa maneno mazuri ambayo mwisho wake yanatuletea kuchanganyikiwa (confusion). Badala ya kumuomba Mungu atupe maisha ya furaha tunampangia maisha tunayodhani yatakuwa mazuri kwetu. Mtume Paulo aliwahi kuomba sana kwamba mwiba umtoke. Jibu la Mungu likawa si kuuondoa mwiba bali kumjulisha kwamba amepewa neema inayotosha kuishi na mwiba huo bila madhara yoyote. 2 Kor 12:7-9 “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”
Nakuombea msomaji wa ujumbe huu kwamba Mungu akupe ufahamu
wa rohoni ili uweze kutambua watumishi wa kweli na kuweza kuchukua hatua
stahiki za kukufanya utimize kusudi la Mungu la kukuweka hapa duniani. Mungu
akusaidie umjue Mungu ili uweze kuwakataa watumishi wa shetani hata kama
unawapenda na kuwakubali watumishi wa Mungu aliye hai hata kama huwapendi.
Mungu akutane na haja ya moyo wako sasa katika Jina la Yesu Kristo!
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)