Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini utaendelea kuishiwa pesa hata kama unaingiza kipato (sehemu ya pili)

Kwa nini utaendelea kuishiwa pesa hata kama unaingiza kipato (sehemu ya pili) – Dr Lawi Mshana

Watu wengi hawaishiwi pesa kwa sababu ya umasikini bali kushindwa kusimamia fedha zao. Kwa hiyo hata wenye uwezo mzuri kifedha wamekuwa wakiishiwa fedha pia. Lazima tujiulize kwanini hata wenye kipato kizuri wanaishiwa pesa.

NB: Katika makala iliyopita nilizungumzia kipengele namba 1 hadi 10.

11. Unatumia pesa nyingi kuliko unazoingiza

Chanzo kikuu cha kufilisika kwa wengi ni kutumia pesa nyingi kuliko pesa anazoingiza. La kufanya hapa ni kupunguza (kubana) matumizi na kuongeza kipato zaidi.Ukipitia vizuri matumizi yako utagundua kwamba kuna matumizi ungeweza kuyaepuka kwa muda na bado  ukaweza kuishi. Lakini pia ungeweza kugundua kwamba zipo njia ambazo zinaweza kukuingizia kipato ingawa hujawahi kuzifanya. La msingi ni kutoka katika maisha ya mazoea unayoyafurahia hata kama hayana msaada kwako (comfort zone).

12. Unawekeza kwenye vitu badala ya kwako mwenyewe

Pengine unanunua vitu vya anasa ambavyo sio vya kiwango chako cha maisha au umepanga kwenye nyumba ambayo sio ya kiwango chako cha maisha. Badala yake ungewekeza zaidi kwenye elimu yako, uwekezaji wa maana na kuweka akiba. Ni aibu kununua vitu vya kifahari lakini hujiwekei akiba wala hujiungi na mfuko wa hifadhi ya jamii.

13. Unajaribu kuwa tajiri kwa haraka

Watu wengi wanatafuta njia ya kuondokana na umasikini kwa kutafuta utajiri wa haraka. Wako tayari kuwekeza zaidi kwenye bahati nasibu na kuhatarisha maisha yao kwa wizi au rushwa kuliko kuwekeza kwenye shughuli zinazoeleweka na kukubalika. Ukifuatilia matajiri wengi utagundua kwamba hawakutajirika kwa siku moja. Mara nyingi tunajikita katika kuangalia mafanikio yao ya leo na kusahau kufuatilia historia ya nyuma kabla ya utajiri wao.

14. Huzingatii bajeti yako

Watu wengi sio tu kwamba hawazingatii bajeti yao bali hata bajeti yenyewe hawana. Unapokosa bajeti pesa zako zinakuwa na walaji wengi wasio rasmi. Uwe masikini au tajiri unahitaji sana bajeti ili ugundue matatizo yako ya kifedha na kuboresha hali yako ya kifedha.

15. Huna mpango wa maisha

Unaishi kwa kutegemea dharura zaidi kwa vile huna mpango wa maisha yako. Vitu vingi unavyogharamia ni vya kushtukiza badala ya mpango kamili. Huwezi kusimamia jambo litokee kwa vile huna mpango thabiti wa maisha. Ukishindwa kupanga, umepanga kushindwa!

16. Unanunua vitu vinavyoshuka thamani

Sababu mojawapo ya watu kuwa masikini ni kununua zaidi vitu vinavyoshuka thamani kama magari, mitumbwi nk. Hali hii inawafanya watu kuwa na raslimali chache za kujenga utajiri na kujikuta wanaishi kwa kutegemea mshahara peke yake. Inafaa kununua zaidi vitu vinavyoongezeka thamani kv ardhi, hisa na biashara ya mtandao.

17. Huko tayari kujitoa kisadaka

Watu wengi wanadhani mafanikio yatakuja kwa kuwa na ujuzi peke yake. Ni asilimia 20 tu ya ujuzi wa kichwani inahitajika kwa ajili ya mafanikio. Sehemu kubwa inahitaji kubadilika kivitendo na kimtazamo ili tufanikiwe. Na wengi hawako tayari kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya mafanikio.

18. Unajaribu kufanya mambo mengi kwa mara moja

Wengi wanakuwa masikini kwa sababu ya uroho wa kutaka kila kitu kwa kipindi kifupi. Unapoamua upate kila unachohitaji kwa mara moja lazima ukwame. Weka vipaumbele vya maisha yako vinavyoendana na raslimali zilizopo. Hutafanikiwa kwa kuamua kulipia masomo ya gharama kubwa na kujenga nyumba wakati huohuo. Fanya jambo moja baada ya jingine.

19. Unalipa kiasi kikubwa kwa ajili ya simu yako ya mkononi

Kuna watu wamenunua simu za bei mbaya wakati wanazitumia kwa matumizi sawa na ya simu ndogo. Mwingine hata internet hajui lakini ana simu ya bei mbaya ili kuringishia watu. Lakini pia kuna watu wanagharamia mawasiliano kwa simu kuliko chakula wanachokula. Na kibaya zaidi simu hizo hazichangii chochote katika maisha yao ya kiuchumi.

20. Hutaki kuongeza ujuzi wala mafunzo

Unaporidhika na kiwango chako cha elimu hata pale fursa za kusoma zinapopatikana, unaendelea kubaki na kiwango chako cha kipato kwa kipindi kirefu. Kadiri unavyoongeza elimu ndivyo, unavyojiweka katika nafasi ya kupata kazi ya maana zaidi na yenye kipato zaidi. Hata hivyo mafunzo si kwa ajili ya ajira peke yake. Unaweza kuwa umeajiriwa na ukaongeza ujuzi wa ufugaji, kilimo, biashara ya mtandao nk.

Post a Comment

0 Comments