Kwa nini utaendelea kuishiwa pesa
hata kama unaingiza kipato (sehemu ya kwanza) – Dr Lawi Mshana
Watu wengi hawaishiwi pesa kwa sababu ya umasikini bali
kushindwa kusimamia fedha zao. Kwa hiyo hata wenye uwezo mzuri kifedha wamekuwa
wakiishiwa fedha pia. Lazima tujiulize kwanini hata wenye kipato kizuri
wanaishiwa pesa.
1. Kufanya maamuzi ya kukurupuka
Unapokuwa kwenye
msongo wa mambo fulani ni rahisi kufanya maamuzi ya kukurupuka na kujikuta
ukiishiwa pesa. Ndiyo maana hata mtu anayetaka kununua vitu madukani
anashauriwa afanye ‘window shopping’ (aende kujua bei akiwa hana pesa mfukoni)
ndipo siku nyingine aende na pesa kwa ajili ya kufanya manunuzi. Bila hivyo
atajikuta akinunua kitu asichohitaji au kwa bei kubwa na baadaye kukikuta duka
jingine kinauzwa kwa nusu ya bei aliyonunulia.
2. Unapuuzia madeni makubwa
Watu wengi hawana mkakati wowote wa kulipa au kupunguza
madeni makubwa. Lazima ujifunze kushughulikia madeni makubwa uliyo nayo kama
unavyoshughulikia madogo. Ukiyapuuzia unafikia mahali unatumia pesa zako kana
kwamba hudaiwi na siku utakapofuatiliwa utakuwa na hali mbaya sana kifedha. Unapopunguza
deni kubwa unaweza kumvutia anayekudai kukusamehe kabla hujalimaliza. Huwezi
kueleweka kama unaendelea vizuri na maisha bila kupunguza kabisa deni la watu.
3. Unajidharau na kujiona mnyonge
Mtu akiwa na ugumu wa kifedha halafu akajidharau, hatafanya
chochote ili kuibadilisha hali yake. Lazima tujue kwamba kuna kazi nyingi mpya
ambazo tunaweza kujifunza leo ambazo zinaweza kubadilisha maisha yetu. Tuache
mazoea ya kufanya kazi zilizofanywa wakati wa mkoloni ambazo hazitatui
changamoto za watu wa leo. Inasemekana wengi wetu hatutumii 10% ya uwezo
tuliopewa na Mungu katika ubongo wetu. Tungeliweza kufanya makubwa ila
hatutumii akili zetu ipasavyo.
4. Hujajifunza kudhibiti fedha zako binafsi
Kuna watu wanakopa bila hata kujua vizuri riba au jinsi
watakavyokatwa na muda wa makato hayo. Matokeo yake mtu analipia deni takriban
mara mbili ya pesa alizokopeshwa. Na kibaya zaidi amekopa kwa ajili ya kufanya
kitu ambacho hakikuwa na uharaka kiasi hicho. Au anajikuta mkopo huo hautoshi
hiyo shughuli yake hivyo anaongeza mkopo mwingine juu yake. Usikope pesa ili
UJIFURAHISHE bali UPATE UHURU WA KIFEDHA katika siku zijazo. Ni kosa kubwa kukopa
mkopo wa riba kwa ajili ya kununua vitu ambavyo havikuingizii wala kuchangia chochote
katika maisha yako.
5. Hujilipi kwanza
Unakuwa masikini kwa vile hujilipi wewe mwenyewe kwanza.
Kujilipa mwenyewe ni kuweka kiasi fulani kama akiba kabla ya kutumia
kilichobaki kwa ajili ya matumizi. Kila unapopata pesa unawaza tu matumizi
lakini kamwe huwazi kuhusu akiba. Kuna mtu aliwahi kusema hapati pesa
zinazotosha kuweka akiba. Lakini mtu huyohuyo ukimfuatilia sana anachangia
sherehe kadhaa kwa mwezi, anahonga wanawake na kununua vinywaji ambavyo
vinadhoofisha kinga ya mwili wake.
6. Unatanguliza furaha ya leo kabla ya mahitaji ya kifedha
ya baadaye (siku zijazo)
Unawaza zaidi jinsi utakavyojifurahisha kwa kutumia pesa
zako leo bila kufikiri kuhusu maisha yako ya baadaye. Jiulize vitu unavyonunua
leo kiasi gani vitakusaidia katika maisha yako ya miaka ya mbeleni. Lazima
uanze kujiuliza nguvu zikipungua au kazi yako ikifikia mwisho itakuwaje ndipo
utaona umuhimu wa kuandaa maisha ya baadaye. Badala ya kununua vipodozi vingi
leo utaanza kuvipunguza ili uandae maisha yajayo.
7. Huna mfuko wa dharura
Huu mfuko wa dharura ni wa kukusaidia ukipata dharura za
maisha, ukiwa mzee (ukistaafu) au ukiondoka duniani (unawaachaje waliobaki).
Kwa hiyo hata kama utakuwa huwezi kufanya kazi unazozifanya leo mfuko huu
utakusaidia. Vinginevyo kiwango chako cha maisha kinaweza kushuka ghafla. Mfuko
huu sio lazima uutunze wewe mwenyewe. Ziko taasisi za mifuko ya hifadhi za
jamii ambazo ziko kwa ajili hiyo.
8. Una matumizi makubwa sana kwenye gharama ya nyumba
Pengine unatumia pesa nyingi sana kwenye kulipia deni la
nyumba au kodi kubwa. Inashauriwa utumie kiasi kisichozidi 20% ya kipato chako
kwenye gharama za nyumba. Huna haja ya kung’ang’ania mjini ikiwa unalipa
gharama kubwa ya nyumba. Na huna sababu ya kukopa kwa ajili ya nyumba kubwa
sana isiyoendana na uwezo wako kifedha.
9. Hujui pesa yako inakwenda wapi
Unaishiwa kwa vile huna bajeti. Kama hujui pesa yako
inakwenda wapi, huwezi kuigeuza ielekee ule upande ambao utakuwa na manufaa
kwako. Unapojua kwamba una pesa za kutosha kushughulikia mahitaji yako yote na
baadhi ya mambo ambayo sio ya lazima sana, unalala usingizi mzuri usiku. Kama
hujui pesa zako zinakwenda wapi, hata kama kipato kitaongezeka hakuna
mabadiliko yatakayotokea kwenye maisha yako.
10. Hutofautishi matamanio (wants) na mahitaji (needs)
Kwa ujumla watu wanapata shida sana kutofautisha matamanio
na mahitaji. Wanatumia neno ‘mahitaji’ takriban kwa kila kitu wanachonunua
wakidhani wanapaswa kufanya hivyo. Unaweza KUHITAJI gari kwa ajili ya usafiri
au KUTAKA/KUTAMANI gari la kifahari ili nawe uonekane tajiri. Mtazamo huu
umeshusha wengi kiuchumi. Tambua unahitaji nini (needs) na unataka nini
(wants).
…..Somo hili litaendelea siku nyingine
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)