Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini una bidii ya maombi lakini hupewi kwa wakati?

KWA NINI UNA BIDII YA MAOMBI LAKINI HUPEWI KWA WAKATI? (Ujumbe wa leo kanisani) – Lawi Mshana Zipo sababu nyingi za kuchelewa kujibiwa maombi. Lakini mojawapo ni kutokukua na kufikia viwango ambavyo Mungu anakuona kwamba unastahili kupewa majibu yako. Kama utapewa kabla ya kukua, baraka zinaweza kukupoteza. Hata mzazi hawezi kumpatia mtoto wake kila anachoomba hata kama atalia kiasi gani. Hata maandiko yanatukataza kumpa mtu wadhifa kama bado ni mchanga kiroho na hajapata uzoefu wa kutosha. 1 Timotheo 3:6 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.” Mungu anataka tugeuzwe kwa kufanywa upya nia (mindset) ndipo tutajua hakika mapenzi ya Mungu. Kwa maneno mengine unaweza kuwa vizuri rohoni, lakini uwe umeharibikiwa kwenye nafsi na kujikuta hupokei majibu yako. Kumbuka kwenye nafsi ndipo tunakuwa na uwezo wa KUFIKIRI, KUAMUA NA KUHISI. Rum 12: 2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Ndiyo sababu mahali pengine Biblia inasema kuna watu wameharibika akili zao. Katika andiko hapo juu neno kugeuzwa “transformed” ni neno la Kiyunani “metamorphoo”, ambapo neno la kingereza “metamorphosis” limepatikana. Tunasema metamorphosis pale kiluwiluwi (tadpole) kinapogeuka kuwa chura (frog) au pale kiwavi (caterpillar) kinapokuwa kipepeo (butterfly) baada ya kupita hatua kadhaa. Hivi ndivyo Mungu anavyotaka mageuzi kwa watoto wake. Sijui uko hatua ipi kwenye mageuzi haya ya Kikristo? - Egg (yai), larva (kiwavi), cocoon/pupa(kifukofuko) au butterfly (kipepeo). UHUSIANO WA UKUAJI WA KIPEPEO NA MAISHA YA MKRISTO 1. Yai (Egg) – Tunakuwa watoto wachanga tunaohitaji ulinzi na malisho 1 Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.” (teknion) – mtoto mchanga. Gal 4:19 “Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;” 2. Kiwavi (larva) – Kiwavi kinatembea taratibu na kula sana muda wote. Hapa tunaanza safari lakini tunalishwa zaidi na kuanza kuacha ya kale na kuachana na marafiki wanaozuia ukuaji wetu. Rum 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (teknon) – mtoto 3. Kifukofuko (cocoon) – Hapa kiwavi kimefikia hatua ya mwisho na kutengeneza koa (shell). Hapa Mungu anajaza pale tulipopoteza tulipoacha ya kale kwa neema yake, upendo na nguvu zake Gal 4:1,2 “Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.” (nepios) - mtoto chini ya mwangalizi 4. Kipepeo (Butterfly) – Hapa kipepeo kinakuwa na mabawa lakini hakijui kama kinaweza kuruka mara hiyohiyo. Kinapoachilia uwezo wake kinaanza kupaa. Hatua hii Mkristo anakuwa na ujuzi alioupata katika kanisa, huduma na malezi ambao akiutumia unaleta mageuzi makubwa. Rum 8:19 “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.” (Huios) – mwana LAKINI PIA KUNA AINA 3 ZA WAUMINI KIBIBLIA – Jigundue wewe ni aina ipi. 1. Mtu wa tabia ya asili – Huyu mtu hajaokoka ila anaweza kujiita mkristo na kutoa sadaka kama wengine. Akikukuta unabubujika kwa maombi na kuishi maisha ya imani hawezi kukuelewa. Mambo hayo kwake ni upuzi. Anaishi maisha ya kidini tu ya kistaarabu lakini hatambui mambo ya rohoni. 1 Kor 2: 14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 2. Mtu wa tabia ya rohoni – Huyu mtu ameokoka na anatambua yote lakini hatambuliwi. Ndugu na marafiki wasiookoka wanampuuza na kumdharau kwa vile amesajiliwa mbinguni ingawa anatembea duniani. Hatafuti kutambuliwa na watu bali kumpendeza Mungu. 1 Kor 2:15 “Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.” 3. Mtu wa tabia ya mwilini – Huyu mtu ameokoka lakini anajiongoza mwenyewe. Amempa Yesu nafasi ndogo sana katika maisha yake. Anaweza kununua nguo za bei mbaya lakini hata Biblia hana, anaenda mikono mitupu kanisani bila daftari, kalamu, Biblia au sadaka. Hatoi zaka wala hashiriki maombi ya kufunga. Mara nyingi anashiriki ibada za Jumapili tu maana katikati ya wiki yuko busy kutafuta pesa na wala hahukumiwi moyoni kwamba amemuacha Mungu. 1 Kor 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini… Ukiangalia kwenye picha utaona mduara unaoelezea maisha yako. MAOMBI Naomba Mungu akuondolee mzigo mzito ulio nao na dhambi zinazokuzinga kwa wepesi ili usije ukaaibika siku ya mwisho. Naomba Mungu akupe hatua nyingine ili ufaidike na wokovu aliotupatiwa kwa gharama ya uhai wa Yesu badala ya kuwa msindikizaji tu ambaye huna badiliko lolote. Mungu akupe macho ya kuona mipango aliyokupangia ili usiishi maisha ya kubahatisha. Pokea maombi haya tunapomaliza mwaka na kuanza ukurasa mwingine katika Jina la Yesu Kristo aliye hai. Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments