KWA NINI HATA WATUMISHI NA WAUMINI WAZURI WAMETAWALIWA NA MADENI NA NI TEGEMEZI WA MISAADA (OMBAOMBA)
Kila mmoja wetu anaweza kukutana na changamoto za maisha zinazomlazimu kukopa. Hata hivyo sio mpango wa Mungu TUTAWALIWE NA MADENI au TUWE WATUMWA WA MADENI.
Napenda kukushirikisha baadhi ya sababu zinazoweza kukufanya wewe kama mtu wa Mungu utawaliwe na madeni na utegemezi.
1. Kutoridhika na baraka zako na kunia makuu
Ebr 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”
Rum 12:3,16 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.”
Fedha sio dhambi. Hata Biblia inatambua umuhimu wa fedha. Mhubiri 10:19b “Na fedha huleta jawabu la mambo yote.” Ila Biblia inasema kwamba dhambi ni TABIA YA KUPENDA FEDHA NA KUTORIDHIKA. Mungu anataka turidhike na vitu tulivyo navyo na kutambua mpango wa Mungu juu ya maisha yetu. Mtu anayenia makuu ni rahisi kutamani kumiliki kitu kabla ya wakati wake. Mfano, mtu kuamua kukopa ili tu amiliki gari wakati hana nyumba, hana uwezo wa kulihudumia gari na wala hana safari za lazima zinazohitaji kumiliki gari. Mungu ameahidi kutubariki lakini pia amesema kila jambo lina wakati wake. Mungu ana wakati wake aliopanga kutuinua. 1 Petro 5:6 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.”
Huna sababu ya kupaua nyumba kwa mabati ya gharama kubwa ili tu watu wadhani una pesa wakati unajua mwenyewe kwamba unaokoteza. Matokeo yake unakosa mahitaji mengine ya msingi. Unaonekana kwa nje u tajiri mkubwa wakati unaogea sabuni ya kufulia kv mbuni au komesha.
2. Kuiga kiwango cha maisha ya watu wengine badala ya kuiga imani.
2 Kor 10:12,13 “Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu.” Mtume Paulo alijitahidi sana kutambua kipimo alichopimiwa na Mungu. Mungu hajapanga kwamba kila mtu awe Rais wa nchi. Ni lazima utambue utainuliwa kuwa nani. Iga imani lakini sio kiwango cha maisha ya mtu mwingine. Tena iga imani ya mtu baada ya kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wake usije ukafa kabla ya wakati wako. Waebrania 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.”
1 Sam 17:38-40 “Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.”
Daudi alipovikwa silaha ambazo hana uzoefu nazo alikataa akachukua zile alizozizoea. Angelazimisha kutumia silaha hizo angeshindwa vita. Jitambue na kutambua neema uliyopewa badala ya kuingilia maisha ya watu wengine. Bwana Yesu hakuhitaji kumiliki mashua au punda bali alipohitaji aliagiza na kutumia. Lk 5:3 “Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.” Lk 19:30-34 “akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda? Wakasema, Bwana ana haja naye.”
Huna sababu ya kusomesha watoto kwenye shule za bei mbaya wakati dalili za kumiliki nyumba binafsi hazipo kwa sababu tu ya kuiga maisha ya watu ambao hujui wana vyanzo vingapi vya mapato.
3. Kutojua kubana matumizi na kutokuwa na matumizi ya lazima
Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.”
Kuna watu kila baraka zinapoongezeka, na matumizi yanaongezeka. Kwa hiyo hakuna wakati watafanya shughuli ya maendeleo zaidi ya kuvaa vikali na kula kwa anasa. Lazima ujifunze kubana matumizi ili ziada unayopata isiishie kwenye chakula na kodi ya pango. Kuna watu wamepanga vyumba viwili kwa miaka mingi lakini kwa siku wanatumia pesa nyingi sana kwa muda wa maongezi (simu) na kula na kunywa mara nyingi kwa siku. Kibaya zaidi wanampigia simu mtu anayekaa nyumba ya pili badala ya kutuma tu mtoto au kwenda kwa miguu kumuona. Kuna watu hawafanyi kazi zaidi ya kupika, kufagia na kuosha vyombo lakini wanakula utadhani wanaenda shamba. Kama wangeamua kwa wiki mbili tu wanywe uji asubuhi bila kitafunio wangeweza kufanya jambo fulani la maendeleo. Kuna watu wangeweza kununua mahindi ya mwaka mzima wakati bei zikiwa nafuu lakini wameamua wanunue zaidi nguo na kuendelea kununua unga kwa kilo au visado na mafuta kwa mijari.
4. Kutoweka vipaumbele na kushindwa kuvisimamia
Lk 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.”
Kuna watumishi wanadhani kumpenda Mungu ni kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Wakati mwingine wanawachosha hata waumini na kuonekana kama hawawajali. Michango haiishi kanisani tena katika miezi ambayo wazazi wanatakiwa walipe ada za watoto wao. Utakuta kuna mchango wa ujenzi na wakati huohuo kuna mchango wa semina na safari za kimisheni. Ingawa Bwana Yesu alisisitiza kuishi kwa imani, alionya kutumia imani kijinga. Alisema tunatakiwa tukae chini na kuhesabu gharama kabla ya kuanzisha mradi au shughuli yoyote kubwa ili tusije tukachekwa kwa kuanzisha vitu ambavyo havimaliziki. Wengine kila wanachofanya kinaishia njiani halafu wanaanzisha kingine. Tatizo watu wengi hawana MPANGO KAZI KATIKA MAISHA hivyo wanaishi BORA LIENDE.
Lazima ujiwekee malengo kwamba mwaka huu utafanya nini na mambo mengine uweze kuyafumbia macho kwa muda. Mimi nafanya kila jambo kwa muda wake. Tujifunze jinsi Mungu alivyoumba mbingu na nchi. Hakuumba jambo jingine mpaka alipoona analolifanya limekamilika kwa uzuri. Mwa 1:12,13 “Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.”
5. Kupendelea mikopo ya riba badala ya kuweka akiba (hasa kwa wale wasio na mshahara rasmi bali wanategemea huruma za watu)
Mit 6:6-9 "Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?" Mungu anasema kwamba kama tumeshindwa kujifunza kwake na kwa wataalamu wa uchumi, tujifunze kwa wadudu kama chungu au sisimizi. Chungu hana mtu anayemsimamia lakini anajituma mwenyewe kuweka akiba ya chakula. Wapo watumishi ambao hawana mpango wowote wa kesho wala kwa ajili ya familia zao pale watakapotwaliwa na Bwana. Kwa vile watumishi wengi wa kiroho wanategemea huruma za waumini, walitakiwa wawe waangalifu sana katika kutegemea mikopo. Ni bora zaidi kama wataweka akiba kidogokidogo ili baada ya miaka kadhaa wafanye wanachotaka kufanya badala ya kukopa ili wakifanye kwa haraka na kisha kudaiwa kwa muda mrefu tena kwa riba. Kuna haja ya kutumia vizuri mabenki na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya maisha ya uzeeni na usalama wa familia kwa ujumla.
6. Kutolipa deni (au kutopunguza deni) kabla ya kupangia pesa zinazopatikana.
Mathayo 18:25 "Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni."
Biblia imeagiza kwamba mtu anayekopa anatakiwa kulipa deni. Zab 37:21 “Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” Mtu ambaye akikopa halipi hata kama anajiita mpakwa mafuta anahesabika kwamba anadhulumu. Mafuta ya Roho Mtakatifu yanavunja nira na mizigo inayolemea watu na sio kuongezea watu vifungo na kongwa shingoni. Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Ingawa kukopa sio dhambi, Biblia haipendekezi kukopa kama njia bora ya kuendesha maisha. Mit 22:7 “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” Unapokopa unakuwa mtumwa wa yule aliyekukopesha. Sababu kuu ya watu kuwa na madeni yasiyolipika ni kutokuwa na mpango wa kupunguza deni kila baraka zinapopatikana. Niliwahi kuzungumzia hili katika makala yangu ya KWA NINI BAADHI YA WALOKOLE WAKIKOPESHWA HAWAREJESHI? Kila unapopata pesa lazima ukumbuke kwamba unadaiwa pesa za watu. Vinginevyo utashindwa kukopeshwa tena au utalazimika kukimbia mji au kubadili line ya simu mara kwa mara.
7. Kutojizoeza kuishi maisha ya imani na kumtegemea Mungu
2 Wakorintho 11:9 “Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.”
Wako watumishi wanakwepa kuishi kwa imani kwa kuamua kuwalemea watu wengine. Ni kweli waumini wana wajibu wa kuwalea watumishi wa Mungu.1 Kor 9:13-15 “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu.” Hata hivyo sio kwa kuwa ‘mizigo’ kwa waumini. Kulemea watu ni kuwa mzigo kwao. Sio mpango wa Mungu kwa mtumishi wa Mungu kuwa ombaomba kwa waumini mpaka wakisikia anapiga hodi nyumbani kwao wanakwazika. Lakini pia ukizoea kuomba pesa na vocha kwa waumini utakosa mamlaka ya kuwaonya wanapokosea. Waache watoe sadaka na zaka kanisani na kumuomba Mungu mwenyewe akuinulie watu wa kukulea. Hata Bwana Yesu hakupewa pesa na kila mtu bali kulikuwa na wanawake kadhaa waliokuwa na mzigo wa kubeba huduma yake kifedha. Lk 8:2,3 “na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”
8. Kukosa ubunifu na kutokuwa wajasiriamali
Mwanzo 2:15 “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.”
Watumishi wengine wana ubunifu katika kuhubiri kanisani na kwenye mikutano peke yake. Upako wao unaonekana tu madhabahuni lakini sio nyumbani. Mungu alipomuweka Adamu katika bustani ya Edeni hakumpa nyumba wala barabara. Alijua amempa roho ya ubunifu na ujasiriamali ndani yake hivyo atagundua saruji nk. Mtume Paulo ambaye ana mashabiki wengi kwamba alimtumikia sana Mungu, hakuhubiri Injili peke yake bali pia alishona hema ili asiwalemee watu. Mdo 18:3 “na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.” Hatuna sababu ya kusema tumeitwa kufanya huduma za kiroho muda wote (full-time ministry) wakati hatuna kazi (hatujatingwa) muda wote bali tunaangalia tu tamthilia na michezo badala ya kuomba, kusoma Neno la Mungu na kuwahudumia watu wake.
9. Kutotembea na wingu
Kutoka 13:21 “Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku.”
Wana wa Israeli waliposafiri kuelekea nchi ya ahadi waliongozwa na wingu mchana na nguzo ya moto usiku (shekinah glory). Wingu liliposimama nao walisimama, lilipoenda taratibu nao walienda taratibu, lilipoenda kwa kasi nao waliongeza mwendo. Wapo watumishi wamepishana na Mungu kwa kulitangulia wingu au kuliacha wingu liende bila wao. Lazima mtumishi ajue Mungu anamtaka afanye nini mwaka huu ili asije akafanya mambo ambayo amepangiwa kuyafanya mwaka ujao na kuacha yale ya mwaka huu. Unapopishana na Mungu lazima pia utapishana na baraka zako. Haitakuwa rahisi kwako kupata 'mana' unapopita katika jangwa la utumishi wako. Kama Mungu alitaka uanze kujenga nyumba yake ndipo ujenge ya kwako binafsi halafu ukafanya kinyume chake lazima upite katika kipindi kigumu. Mtu aliyelaaniwa anaweza kujenga nyumba na asinufaike nayo. Kum 28:30 “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.” Mtumishi aliyelaaniwa anakuwa na waumini wenye uwezo kifedha lakini hawamkumbuki.
10. Kutotoa zaka ya kila baraka na kutotoa sadaka
Malaki 3:8-10 "Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili loteLeteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.”
Kuna watumishi ni mafundi wa kuhamasisha waumini wao watoe zaka kamili lakini wao wenyewe hawatoi. Matokeo yake waumini wanapotii wanabarikiwa na watumishi waliowafundisha wanaendelea kupigika kiuchumi. Watumishi wengine hata hawaoni aibu kutotoa sadaka ibadani. Utadhani wao ndio Mungu anayepewa hizo sadaka. Mungu anataka tutoe zaka (fungu la kumi) ya kila baraka tunayopata na sio pesa peke yake. Kama umepata baraka ya kitu ambacho ni vigumu kukigawa ili kutoa zaka yake, kithaminishe na kutoa zaka yake. Mfano kama ni kuku na ana thamani ya sh 20,000, toa sh 2,000 kama zaka. Pia jipangie kiwango cha sadaka kwa kila ibada kinachoendana na hali ya sasa ya uchumi na uwezo wako kifedha. Na kama kuna siku hukwenda kanisani, siku ukienda toa pamoja na sadaka ya siku ambayo hukwenda. Pengine unashangaa hili ninalolisema lakini lina ukweli ndani yake. Hivi ukisafiri miezi miwili ukafunga chumba chako ulichopanga, siku ukirudi hutalipa kodi ya pango? Hivi ukifunga duka lako kwa mwezi mmoja siku ukilifungua hutalipa kodi ya mapato? Kama duniani tunafanya hivi, Je kwenye serikali ya Mungu wetu?. Tunatakiwa kufanya zaidi katika Ufalme wa Mungu wetu. Mathayo 5:20 “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”
11. Kutotumikisha karama iliyo kuu ndani yako
Warumi 12:6 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani.”
Bwana Yesu alitoa huduma tano kwa ajili ya kulikamilisha kanisa lake. Efe 4:11,12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.” Mtumishi wa Mungu hatapata upenyo kamili katika maisha yake kama anatumika katika huduma ambayo ni ndogo (minor) na kuacha huduma kubwa aliyopewa (major). Kama dhehebu limempa uchungaji wakati Mungu amempa utume na akaamua kuchunga kanisa peke yake hatakuwa na upenyo kamili. Sio lazima aache uchungaji lakini lazima aichochee na kuitumikisha huduma iliyo kuu ndani yake. Mtumishi anapotumika kwenye huduma ambayo haina baraka zake au upenyo wake, lazima atakuwa omba omba na tegemezi ili aweze kuishi. Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!” Swali la kujiuliza ni Je, Ni Bwana amekutuma kufanya hiyo huduma unayoifanya?
12. Kuwa na ngome na madhabahu zinazokutesa
Ku 3:21,22 “Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu; Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.”
Kama mtumishi ana ngome ambazo hazijaangushwa maishani mwake, atakuwa mzuri tu madhabahuni lakini shetani hatamruhusu kuwa na maisha ya mafanikio kifamilia na kimaisha. 2 Kor 10:4,5 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.” Hakuna mtu anaweza kufanikiwa katika maisha kama shetani amepandikiza mtazamo potofu ndani yake na kisha akauamini. Mara nyingi mtazamo huu wa kushindwa unatokana na maagano yaliyofanyika katika madhabahu za ukoo ambayo hayajafutwa kwa damu ya Yesu tangu mhusika alipompokea Yesu. Ngome hizi zinaweza kumfanya mtumishi hata kama ana waumini wengi wenye uwezo bado awe na kipindi kigumu sana kiuchumi. Ngome zikiangushwa zinakupa kibali hata kwa wasiomjua Mungu. Mungu aliwapa watu wake kibali (kufadhiliwa) kwa Wamisri mpaka wakawapa fedha na dhahabu. Kutoka 11:3 "Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri." Unapomtumikia Mungu katika ufalme wake atakuinulia watu kwa ajili ya maisha yako. Isaya 43:4 “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.”
Mungu akuponye wewe ambaye ujumbe huu ni kwa ajili yako. Lakini pia Mungu akutumie kuwa msaada kwa watu wengine wenye shida za aina hii katika Jina la Yesu aliye hai.
Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255-712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania
Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)