KUNENA KWA LUGHA YA ROHO MTAKATIFU – Dr Lawi Mshana
Kama umenifuatilia vizuri nilipoandika kwamba UPENTEKOSTE
SIO DHEHEBU BALI NI MFUMO WA MAISHA utagundua kwamba sijasema upentekoste
haupo. Nilichosema ni kwamba huwezi kuufungia upentekoste kwenye dhehebu
fulani. Na nimejitahidi kuonyesha mapungufu yaliyopo ili upentekoste urudi
mahali pake. Napenda tutambue mambo muhimu mawili:
1. Mbinguni hakuna kitabu cha madhehebu
bali kuna KITABU CHA UZIMA ambapo yameandikwa majina ya waliompokea Yesu. Ufu
20:15 “Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima,
alitupwa katika lile ziwa la moto”.Ufu 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe
cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale
walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.” Lakini pia mtu anaweza
kufutwa kama atamuacha Bwana. Ufu 3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi
meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri
jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”
2. Hakuna dhehebu linalopaswa kudharau jingine kwa kujiona
ni la kwanza au la mwisho kwa vile majina ya madhehebu yetu hayapo kwenye
Biblia wala katika historia ya madhebu ya kwanza. Mimi najua madhehebu yaliyoandikwa
kwenye Biblia ni Mafarisayo, Masadukayo nk.na mengine ya zamani ni Essenes na
Zealots. Pia wafuasi wa Yesu waliitwa “Njia”(Mdo 9:2) na baadaye wanafunzi wa
Antiokia wakaanza kuitwa “Wakristo” (Mdo 11:26). Maana ya Mkristo ni mtu
aliyempokea Kristo na anayeishi kama Yeye. Kwa vile leo kumekuwa na wakristo waliopokea
au kurithi dini tu imebidi tuongeze neno jingine – WAKRISTO WALIOOKOKA. Lakini
kibiblia hakuna mkristo ambaye hajaokoka. Kimsingi madhehebu yanatusaidia tu
tutambuane tunaofanana misingi fulani ya imani na serikali itambue uhalali wetu
wa huduma na makusanyiko.
Upentekoste ulipoanza haukuwa na mipaka. Baadaye watu
wakaanza kutofautiana katika kuweka uzito katika mafundisho fulani fulani.
Mfano wengine walisema la msingi umpokee Yesu lakini hakuna ulazima wa kuombewa
Roho Mtakatifu. Wengine wakasema unaweza kuombewa Roho Mtakatifu lakini sio
lazima unene kwa lugha nk.
Katika somo lililopita nilisema kwamba msingi wa
Upentekoste ulikuwa ni kurudisha umuhimu wa Roho Mtakatifu katika Kanisa la
Mungu. Ilifika mahali watu wakawa wanakariri tu maandiko lakini hawamuhitaji
Roho Mtakatifu. Watu walisahau kwamba walioandika Biblia waliongozwa na Roho
Mtakatifu hivyo na sisi tunaoisoma lazima tuwe na Roho Mtakatifu ili tusiisome
kama gazeti.
TOFAUTI YA KUNENA KWA LUGHA NA AINA ZA LUGHA
Watu wengi wanapinga kunena kwa lugha kwa sababu kuu tatu:
1. Hawajaokoka kwa hiyo kwao masuala ya rohoni ni mageni
sana maana yanatafsiriwa kwa jinsi ya rohoni. 1 Kor 2:14 “Basi mwanadamu wa
tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi,
wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 1 Kor 3:1
“Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya
rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga
katika Kristo.”
Kuna watu aina tatu duniani kwa mujibu wa maandiko
niliyonukuu hapo juu:
(i). Mtu wa tabia ya asili – Huyu mtu anajiongoza mwenyewe
na Kristo yuko nje (1 Kor 2:14). Kwa kifupi hajaokoka.
(ii) Mtu wa tabia ya mwilini – Huyu mtu amempokea Yesu
lakini hajampa nafasi amuongoze hivyo anaishi kimwili (1 Kor 3:1). Ameokoka
lakini bado tabia za mwilini zipo.
(iii) Mtu wa tabia ya rohoni – Huyu mtu amempokea Yesu na
amempa nafasi ya kutawala maisha yake. Yesu kwake sio Mwokozi tu bali pia ni
Bwana wa maisha yake (1 Kor 3:1).
Kwa hiyo mtu asidhani kwamba kwa vile amebatizwa na kupata
kipaimara ni lazima awe mkristo. Lakini pia tutambue kwamba mtu anaweza kuokoka
lakini bado awe na tabia za mwilini. Usiache kuokoka kwa kutazama walioshindwa.
Wapo wengi walioshinda. Hata shuleni hutasoma kama utaangalia wanaofeli. Lazima
siku zote wawepo wanaofaulu na wanaofeli. Ndiyo maana katika kila kanisa la
Ufunuo wa Yohana imeandikwa ASHINDAYE na sio AOKOKAYE. Maana yake ni kwamba kuokoka
ni mwanzo wa safari na lengo ni kushinda. Ambaye hajaokoka bado hajaanza safari
hivyo hawezi kujua ndani kuna mambo gani mpaka atakapoingia kwenye safina.
2. Wengine wanapinga kunena kwa lugha kwa vile hawajajaliwa
kipawa hicho. Kwa vile mtu ameokoka na haneni kwa lugha, badala ya kumlilia
Mungu apewe kipawa hiki anaanza kukikosoa. Utakuta anasema, Mbona fulani
ananena kwa lugha lakini haeleweki? Mbona Mungu ananitumia sana ingawa sineni
kwa lugha? Nk. Kunena kwa lugha hakuna uhusiano wa moja kwa moja na tuhuma
tunazowapa wanaonena kwa lugha. Mtu anaweza kusema kwa lugha ya kabila lake na
za malaika na asiwe na upendo lakini hilo halifuti umuhimu wa lugha. 1 Kor 13:1
“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa
shaba iliayo na upatu uvumao.” Tutaingia mbinguni kwa TUNDA LA ROHO na
tutalipwa mbinguni kwa KARAMA ZA ROHO. Hivyo tukishampokea Yesu tuzingatie yote
mawili ili tukakae pazuri kwa vile hata mbinguni watu watatofautiana utukufu.
3. Wengine hawajui tofauti ya kunena kwa lugha na aina za lugha. Kunena kwa lugha ni kwa ajili ya MAWASILIANO NA MUNGU (nitafafanua zaidi) na aina za lugha ni moja ya karama za Roho Mtakatifu kwa ajili ya UJUMBE KWA KANISA (1 Kor 12:8-10). Mtu mwenye karama ya aina za lugha anaweza kunena kanisani ujumbe ambao unatakiwa mwenye karama ya kutafsiri asimame naye atafsiri kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Hapa sizungumzii wakalimani wa kingereza na Kiswahili! Na ndio maana Biblia ikasema kama hakuna mtu wa kutafsiri afadhali anyamaze katika kanisa 1 Kor 14:27,28 “Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.” Lakini pia mtu mwenye karama hii anaweza kusema lugha ya mtu anayetakiwa kupata ujumbe bila yeye kuijua. Hili lilitokea siku ya Pentekoste wakati Mungu alipotaka watu wa mataifa mbalimbali wapate ujumbe kwa vile waliojazwa Roho Mtakatifu hawajui lugha zao. Mdo 2:6 “Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.”
FAIDA ZA KUNENA KWA LUGHA
Ni kweli kwamba shetani anajitahidi kuiga kila kitu anachofanya Mungu ili kupotosha watu wake. Na ndiyo maana kuna waalimu wa kweli na wa uongo, manabii wa kweli na wa uongo, wachungaji wa kweli na wa uongo nk. Hivyo hutakosa pia watu wanaonena kwa lugha za mapepo. Lakini kunena kwa lugha za mapepo hakuondoi ukweli kwamba ipo lugha ya Roho Mtakatifu. Wanaodanganyika ni wale ambao hawajui kupambanua roho. Mungu ametoa vipawa vya kusaidia kubaini matendo feki ya kishetani. Leo hii kuna watu ambao katiba za madhehebu yao zinasema tunatambua huduma tano za Yesu Kristo (Efe 4:11) – mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu lakini mtu akitoa unabii badala ya kuupima wanamtoa nje ya kanisa. Biblia inasema katika Mithali 14:4 “Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.” Maana yake ni kwamba kama tunataka utulivu kwa kuogopa kwamba karama za Roho zitatumiwa vibaya tuache kufuga ili zizi liwe safi. Ila zizi litakuwa safi bila maziwa. Lakini kama tunataka kunufaika na karama za Roho tufuge lakini tujiandae kupata maziwa na kinyesi pia. Tunywe maziwa na kinyesi tutupe shambani.
Sio lazima upokee kunena kwa lugha siku ya kwanza unapoombewa. La muhimu uwe na kiu na kujiona unakosa kitu muhimu na ndipo siku moja utajazwa. Baada ya kusoma fundisho hili naamini wewe uliye mnyenyekevu utapokea kunena kwa lugha na siku moja utanijulisha kwamba umepokea hata ukiwa peke yako.1 Kor 14:1 “Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.” Ni lazima UTAKE SANA (UWE NA KIU NA SHAUKU) ndipo utapokea.
1.Unaponena kwa lugha husemi na watu bali unasema na Mungu. Hakuna sababu ya mtu kusikia unachosema kwa vile husemi naye. Hivi mimi nikikukuta unaongea na mtu kwenye simu kwa lugha ya kabila lenu nakasirika kwa sababu gani wakati huongei na mimi?1 Kor 14:2 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”
2. Unaponena kwa lugha unanena mambo ya siri katika roho yako (1 Kor 14:2). Ukizama zaidi utagundua kwamba kama ungesikiwa ukiomba kila kitu kwa Kiswahili ungeweza kuuawa au kutoeleweka vizuri. Hebu fikiria umekuja kuniona nikuombee baraka halafu Roho Mtakatifu ananiambia usimuombee kwa vile ni mimi nimeruhusu apitie hali hiyo mpaka atakapotubu Nikiomba kwa Kiswahili kwamba usipokee hutanielewa kabisa. Kwa hiyo nitaomba kwa kunena kwa lugha ili Roho mwenyewe akuombee inavyostahili. Unaweza kupokea toba ya ajabu na kisha baraka zako zije baadaye.
3.Unaponena kwa lugha unajijenga mwenyewe. Ni jambo la kusikitisha kwamba wengi waliopewa neema hii hawaitumii kujijenga bali wanaendelea kuomba kwa Kiswahili au kwa lugha za duniani hata wakiwa peke yao.1 Kor 14:4 “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.” Hata Mtume Paulo aliwahi kusema nikiwa kanisani napenda kuongea kwa lugha mnayonisikia lakini nikiwa peke yangu (katika maombi) nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote. 1 Kor 14:18 “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote.” Shida ni pale tunapokuwa tunakusikiliza uombe peke yako halafu wewe unanena kwa lugha kana kwamba tunaomba maombi ya pamoja. 1 Kor 14:5,6 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa. Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?”
4. Unaponena kwa lugha unaomba katika roho na akili hazifanyi kazi. Unapoomba kwa kutumia akili utaishiwa maneno kwa vile lugha zetu za duniani hazina maneno (vocabulary) za kutosha. Ndio maana mtu akikosa maneno ya kuelezea kitu kilichomfurahisha au kumhuzunisha anaamua alie tu. Lakini lugha ya Roho Mtakatifu haiishiwi maneno. 1 Kor 14:14,15 “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.”
5. Unaponena kwa lugha unashukuru inavyotakiwa. Nikupe mfano, ikiwa umeenda shambani halafu kulikuwa na nyoka ambaye hukumuona hivi utashukuru kwa ulinzi wa Mungu? Unaweza usishukuru kwa uzito kwa vile hukumuona. Lakini Roho Mtakatifu anajua na atashukuru inavyotakiwa. Ingawa anayekusikiliza hajengwi lakini wewe unashukuru vema. Hivyo usinene wakati watu wanasikiliza sala yako ya kuombea chakula kwa vile watashindwa kusema Amen kwa vile hawakusikia ulichosema. 1 Kor 14:16,17 “Kwa maana wewe ukibariki kwa roho, yeye aketiye katika mahali pa mjinga ataitikaje, Amina, baada ya kushukuru kwako, akiwa hayajui usemayo? Maana ni kweli, wewe washukuru vema, bali yule mwingine hajengwi.”
6. Unaponena kwa lugha unaweza kujizuia inapobidi. Nimewahi kwenda kanisa moja nikakuta mtu fulani watu wakimaliza kuomba yeye ndio anaanza kupaza sauti. Nikamkemea kwa vile niligundua anataka tu kujionyesha kwamba anajua sana kuomba. Unaweza kujizuia ili usipishane na wengine labda kama kuna ujumbe Mungu anataka kuuleta kwa kanisa.1 Kor 14:32,33 “Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.” Ila usizuie kunena bila sababu za msingi. 1 Kor 14:39,40 “Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.”
TAHADHARI
Wapo watu ambao lugha yao haibadiliki maneno. Tangu aokoke hapati maneno mengine hata kama anaombea jambo tofauti. Hii ni lugha ya mazoea ambayo inaweza kubaki kwa mtu hata kama Roho Mtakatifu amemhama. Unajua hata kama leo kabila langu watanifukuza hawataweza kuchukua lugha yangu? Hata shetani hakunyang’ang’anywa vipawa vyake ndio maana anavitumia kwa utukufu wake mwenyewe. Utakuta mtu akiombea kanisa anasema RIKABABASAI, akombea mchungaji wake RIKABABASAI, akiombea familia yake RIKABABASAI. Hapa nina mashaka. Ni vizuri kila wakati upewe maneno mapya mpaka mwenyewe ushangae leo nimeombea jambo gani jipya?
Mungu atusaidie tusikosoe mambo tusiyoyajua ili tusije tukajiongezea hukumu siku ya mwisho. Yakobo anatuonya katika Yak 3:1 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.” Mhu 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.” Jambo lolote unalojiona u mjuaji kuna siku utaulizwa uelezee ulilitoa wapi. Hivyo tuwe radhi na vile tulivyo navyo na kuomba tuongezewe neema zaidi. Fanya lile ulilofunuliwa. Kama bado ni siri kwako, hutakiwi ulizungumzie wewe. Mungu atamuinua mwingine aliyempa neema hiyo. Kum 29:29 “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.”
Kumbuka sijaeleza kila kitu kuhusu
kunena kwa lugha. Hivyo kasome Neno la Mungu na kumuomba Roho Mtakatifu
akusaidie kuelewa zaidi.
0 Comments
Karibu sana na ujisikie huru kushirikisha mawazo yako au kuuliza swali tujifunze pamoja (Welcome and feel free to share your thoughts or ask questions so we can learn together)