Ticker

6/recent/ticker-posts

Jinsi ya kushinda utegemezi katika maisha na huduma

JINSI YA KUSHINDA UTEGEMEZI KATIKA MAISHA NA HUDUMA 

Hakuna mtu anaweza kujitegemea kwa kila kitu maana tu viungo katika mwili wa Kristo. Hata hivyo tunaweza kuishi kwa kujitegemea na kuepuka utegemezi, madeni yasiyolipika na mikopo isiyo na ulazima. 

1. Ridhika na baraka zako na usinie makuu 

Ebr 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Kuridhika sio kutosheka. Ingawa bado unatafuta unatakiwa uridhike na vitu ulivyo navyo ili usije ukamkosea Mungu.Unaweza kuishi kwa furaha hata kama kuna vitu bado hujavipata kama wenzako. Wakati mwingine tunahangaika kutafuta vitu ambavyo sio mahitaji yetu bali ni sababu ya kunia makuu. Tunania makuu pale tunapotafuta kuishi maisha ambayo hatukupangiwa na Mungu. Mungu ana mpango binafsi kwa kila mmoja wetu. Rum 12:3,16 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.” Mfano: Si kila mtu anatakiwa apaue nyumba yake kwa mabati ya gharama kubwa wakati hata uhakika wa kumaliza ujenzi mapema haupo. 

2. Usiige kiwango cha maisha ya watu wengine bali ujitambue. 

Mtume Paulo alijitahidi sana kutambua amepangiwa nini na Mungu bila kujilinganisha na watu wengine. 2 Kor 10:12 –16 “Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.” Tumia silaha unazozijua vizuri kama alivyofanya Daudi wakati wa kumuua Goliati. Daudi alivua silaha ambazo hana uzoefu nazo akatumia anazozijua na Mungu akawa upande wake. 1 Sam 17:38-40 “Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.” Mf Si kila mtu atafurahia maisha kwa vile tu anamiliki gari. Wapo walioiga watu na kujikuta wakifilisika au kushindwa gharama za uendeshaji. Lakini pia sio kila mtoto atafanikiwa maisha kwa kusomeshwa shule za kimataifa. Kila mtu afanye kwa kuzingatia uwezo wake na wa mtoto wake na si kwa kuiga maisha ya familia zingine ambazo hajui vyanzo vyao vya mapato yao vikoje. 

3. Bana matumizi na kuwa na matumizi ya lazima 

Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.” Kuna watu wanapata pesa vizuri lakini tatizo lao ni kushindwa kubana matumizi. Chakula kilichotakiwa kutosheleza kwa wiki moja kinaisha kwa siku tatu kwa vile kinapikwa kingi na kumwagwa. Kuna watu hawajui bajeti wala mahitaji yao ya msingi kwa wakati huu. Totafautishe mahitaji ya lazima na mahitaji yasiyo ya lazima (ya anasa). Mfano: Kuna watu wamepanga nyumba zenye vyumba ambavyo hawavihitaji. Wangeliweza kukaa nyumba ya vyumba viwili badala ya vinne na kiasi kinachobaki kikafanya mambo mengine. Laki pia kwa pesa wanazopata wangeweza kununua vitu kwa bei ya jumla badala ya rejareja kv unga kwa visado na mafuta kwa mijari. Bajeti ya vitafunio asubuhi inaweza kupunguzwa kwa muda ili kuweza kukamilisha mambo ya msingi kv ujenzi, masomo nk. 

4. Weka vipaumbele na kuvisimamia 

Lk 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.” Mara nyingi Bwana Yesu ametufundisha imani lakini hapa anatufundisha kuwa na mipango thabiti. Anatuambia kwamba tuwe na mpango (kujenga mnara) na tupige mahesabu kabla ya kuanza mradi wowote ili tusije tukachekwa kwa kushindwa kuumaliza. Hatutaweza kufanya hivyo kama hatuwezi kuweka vipaumbele na kuvisimamia. Tusifanye mambo lukuki kwa muda mfupi na kwa kutegemea raslimali chache zilizopo. Lazima tutaishia njiani. Mfano: Mimi niliwekeza kwenye elimu nikapata shahada ya uzamivu (udaktari) kabla ya kufikia umri wa miaka 40 tena bila mkopo. Kipindi chote hicho niliweza kununua bati bila kuwa na kiwanja. Ndipo baada ya hapo nikaanza ujenzi. Kusoma kwangu kukarahisisha ujenzi baadaye. 

5. Weka akiba na kusubiri badala ya kukopa na kudaiwa kwa riba 

Watu wengi wanateswa na mikopo kwa vile tu wana haraka zisizo na ulazima. Kuna watu wengeweza kununua vifaa taratibu kwa mwaka mzima na kisha kujenga nyumba bila kulazimika kurejesha mkopo wa riba kubwa. Kibaya zaidi kuna wengine wana tabia ya kukopa kwa imani bila kuwa na chanzo chochote cha kipato cha uhakika. Biblia inatuasa tujifunze kwa wadudu kama sisimizi wanavyojipanga kwa kuzingatia misimu. Tujifunze kuweka akiba hata kama kipato chetu ni kidogo. Mit 6:6-9 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?” Mfano: Nimejifunza kwamba kama mtu anaweza kulipa kodi ya nyumba hashindwi kujiwekea akiba benki na katika mifuko ya hifadhi za jamii kv NSSF au kumfungulia mtoto akaunti na kumuwekea kidogo kidogo. Kutofanya hivi kunatusababisha tushindwe kukabiliana na dharura za maisha. Mifuko ya jamii inatoa misaada kwa wateja wake pale wanapofikia uzeeni au matatizo yanapotokea kama kufariki, ulemavu nk. Sio lazima tusubiri tukiajiriwa ndipo tuwekewe pesa kwenye mifuko ya jamii. 

6. Lipa deni (au punguza deni) kabla ya kupangia pesa unazopata. 

Bado sio za kwako. Watu wengi wana tabia ya kuzipangia pesa wanazopata na kusahau kwamba wana madeni. Kama hatuwezi kulipa deni lote lazima tuwe na mkakati wa kulipunguza. Kutojali madeni kunaweza kuleta aibu ukiwa bado duniani au hata baada ya wewe kuondoka duniani. Wengi wamedhalilika na wengine kulazimika kuuza miili yao kwa sababu ya kushindwa kulipa madeni. Mathayo 18:25 “Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.” Unapopoteza uaminifu hutapata pa kukopa tena wala hutakopeshwa tena. Lakini pia utakosa uhuru na kuharibu sifa ya jina lako. Unapokopa lazima ukubali kwamba u mtumwa wa yule aliyekukopesha. Mithali 22:7 “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” Mfano: Kama kuna changamoto imetokea ukalazimika kuazima pesa mahali, unapofanikiwa rudisha hiyo pesa kwanza ndipo upangie pesa iliyobaki. 

7. Jizoeze kuishi maisha ya imani na kumtegemea Mungu Maisha ya imani hayatokei tu. 

Ni lazima tujifunze kama tunavyojifunza kufunga na kuomba. Tunaweza kujikana nafsi na kuishi kwa furaha hata kama hatuna kila kitu tunachohitaji. Mtume Paulo alijilinda sana asiwalemee watu katika huduma yake. 2 Wakorintho 11:9 “Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.” Unapowalemea watu unakosa ujasiri na mamlaka kama u mtumishi wa Mungu. Ni vizuri zaidi kukimbilia kwa Bwana kuliko kukimbilia kwa wanadamu. Mfano: Sijawahi kuomba washirika pesa au vocha nikiwa kanisani kwangu au ninapofanya semina kwenye makanisa mbalimbali. Nashirikisha kanisa zima kwa mahitaji maalum kv safari za huduma nk. Unapokuwa ombaomba unapoteza utisho wa Mungu na heshima kwa watu. 

8. Uwe mbunifu na mjasiriamali 

Hakuna andiko linalotulazimisha kutegemea sadaka hata kama tu watumishi wa Mungu. Mtume Paulo alionyesha wazi kwamba hata kama ni haki yake kuhudumiwa na kanisa hapendi kufungwa na utaratibu huo. 1 Kor 9:14,15 “Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu.” Lakini pia Mungu alimheshimu Adamu kwa kumpa wajibu wa kuitunza bustani ya Edeni. Mwanzo 2:15 “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” Mungu hakumjengea Adamu nyumba wala barabara. Kazi ni heshima. Ndiyo maana hata kama utawaambia watu umefanikiwa kimaisha bado watakuuliza au kujiuliza, “Unafanya kazi gani?” Mfano: Tangu nianze huduma nimeanzisha miradi mbalimbali ili nisilemee watu ninaowahudumia kv kurikodi kanda za mahubiri, darasa la kompyuta, duka la tibalishe, studio, steshenari, duka la rejareja nk. Wala miradi hii haijaathiri muda wangu wa huduma kwa vile nimekuwa nikiwatumia watu kuzisimamia. 

9. Nenda na wingu 

Wana wa Israeli waliongozwa na nguzo ya wingu mchana na nguzo ya moto usiku. Katika safari hii ya kiroho hatuko peke yetu. Utukufu wa Mungu umetuzunguka pande zote. Kutoka 13:21,22 “Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.” Mungu ana mipango aliyotupangia hivyo lazima tujue kalenda yake ili tusilazimishe majibu yake. Mfano: Roho wa Mungu aliniambia nijenge kanisa kama vile ninajenga nyumba yangu binafsi. Nilipofanya hivyo na kuwa tayari kuuza friji na godoro langu ninalolalia ndipo pesa zikapatikana. Nikajikuta naelekezwa kwa wafadhili wenye baraka zetu (samaki wenye shekeli). Kila nilipochukua hatua za kumtii Mungu na kusimamisha mambo yangu binafsi kwa ajili yake, nilipata upenyo wa ajabu sana. Tusipende kutangulia wingu bali tuende na kasi ya wingu (uongozi wa Mungu). 

10. Kuwa na mifuko tofauti tofauti (bahasha tofauti) na kuziheshimu. 

Siku moja nilimuomba Mungu aniwezeshe kupata pesa za kununulia vitendea kazi mbalimbali vya kazi yake. Roho Mtakatifu akanifundisha kupitia maandiko matakatifu. Yohana 13:29 “Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.” Nikajifunza kwamba Bwana Yesu alikuwa na mfuko wa sikukuu na mfuko wa kusaidia maskini. Alipotaka kuandaa pasaka hakuhitaji kukopa au kuomba michango bali aliwatuma tu wanafunzi wake wakaandae gorofani. Tunashindwa kusaidia wasiojiweza kwa vile hatuna mfuko huo wala mpango huo. Mf Nilipopata ufunuo huo nikaanzisha bahasha ya kununulia TV set kwa ajili ya huduma. Kweli nikaweza kuinunua mwaka 1998 na kuonyesha video za Neno la Mungu maeneo mengi kabla sijapata LCD projector. Tangu tuanzishe bahasha za majukumu tofauti kv mfuko wa jamii, mfuko wa utawala, matengenezo, umisheni nk tumejikuta tukifanikiwa kuyatimiza mambo hayo bila shida. Changamoto ya wengi ni kuweza kuheshimu hizo bahasha alizozipangia majukumu tofauti tofauti. Unaweza kufungua akaunti benki ili iwe rahisi zaidi kama mazingira yako yanaruhusu kufanya hivyo ili pia usikae na kiasi kikubwa cha pesa nyumbani. 

Dr Lawi Mshana, +255712-924234, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments