Ticker

6/recent/ticker-posts

Jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia


JINSI YA KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Ukatili wa kijinsia ni tendo analotendewa mtu mwingine bila ridhaa yake ambalo linajumuisha makosa ya kujamiiana bila ridhaa (kubaka), jaribio la kujamiiana bila ridhaa, kumgusa kijinsia pasipo ridhaa au kutomasa (kumgusa mtu sehemu asizotaka), na unyanyasaji bila kugusana (k.m. vitisho vya kutumia nguvu kijinsia, kubugudhi kwa maneno ya kijinsia). 

Mara nyingi waathirika wakuu wa ukatili wa kijinsia ni wanawake, wazee na watoto. 

Hatua za kuchukua Ukatili wa Kijinsia unapotokea: 

1. Watu walio katika uhatarishi au waliofanyiwa ukatili wanatakiwa kutafuta mahali salama mara moja (kwa jirani, ndugu, viongozi wa dini, viongozi wa kijiji au polisi). 

2. Watu waliofanyiwa ukatili wanatakiwa kumjulisha mara moja mtu anayeaminika au kuwasiliana na polisi. 

3. Haraka iwezekanavyo, mwathirika wa ukatili anatakiwa kuripoti kwenye zahanati/kituo cha afya/ hospitali. Kama ni ukatili wa kingono, inashauriwa kwamba mwathirika wa ukatili huo asioge kwa vile kwa kufanya hivyo ataharibu ushahidi unaotakiwa kuchukuliwa. Kama inawezekana, mwathirika wa ukatili asibadili nguo. Kama ni lazima kubadili nguo, aweke nguo chafu kwenye mfuko wa karatasi au kufunga kwenye gazeti, LAKINI SIO mfuko wa plastiki. Kama inawezekana, aliyefanyiwa ukatili asubiri kwenda choo kidogo au kikubwa mpaka afike kituo cha afya. Muathirika atumie vifaa visafi anapoweka choo kama alishindwa kusubiri hadi kituo cha afya. 

4. Ripoti mara moja kwenye kituo cha afya kwa ajili ya huduma ya haraka ya afya. 

5. Katika kituo cha afya, ripoti mapokezi. Usisubiri kwenye mstari. Chukua kadi na ripoti kwa mhudumu wa afya mara moja. 

6. Waathirika wa ukatili wa kijinsia wanatakiwa kuripoti kwenye taasisi yoyote inayotoa huduma za ukatili wa kijinsia (k.v. kituo cha afya, dawati la jinsia (polisi), nyumba salama, vituo (drop in centre), ustawi wa jamii). Kama mwathirika ataripoti kwanza kituo cha afya; atatakiwa kupatiwa matibabu kabla ya kutoa maelezo dawati la jinsia (polisi) na baada ya hapo ataripoti kwenye kituo cha polisi. Kama ataripoti kwanza polisi baada ya hapo anatakiwa kwenda kwenye kituo cha afya. 

7. Kama utakwenda kwanza polisi, hakikisha kwamba unatembelea kituo cha afya/hospitali mara moja au ndani ya masaa 72 tangu uhalifu ufanyike. 

8. Ukiwa polisi, ripoti tukio, toa maelezo na pata fomu ya PF3. Fomu ya PF3 inatolewa bure. 

9. Kabla hujasaini maelezo yoyote kwenye kituo cha polisi, soma kwa uangalifu kuhakiki yaliyoandikwa. 

10. Waathirika wanatakiwa kuwaachia polisi ushahidi wowote (mfano, nguo) ili utumike kwa ajili ya kesi ya jinai dhidi ya mkosaji. 

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments