Ticker

6/recent/ticker-posts

Hatari ya kuishi maisha ya mtu mwingine

HATARI YA KUISHI MAISHA YA MTU MWINGINE – Dr Lawi Mshana Nimependa kukushirikisha ujumbe niliouhubiri leo kwenye kanisa ninalochunga hapa Korogwe. Naamini Mungu hataki hata wewe uishi maisha ya mtu mwingine kwa vile Mungu ana mpango binafsi na wewe. 1. Unashindwa kujua agizo lako (mandate) au maelezo ya kazi yako (job description) Isa 61:1-3 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao; kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.” Bwana Yesu alijua amekuja duniani kufanya nini na maelezo ya kazi yake yalikuwa bayana. Hakuna mtu anapewa kazi katika ofisi bila kupewa maelezo kuhusu kazi yake (JD). Kama hujui unaweza kufanya kazi ya mwingine na kuacha ya kwako na kujikuta mwisho wa siku hulipwi ingawa umetoka jasho kama wengine. 2. Unapoteza kusudi la maisha na upako au mamlaka ya ki-Mungu Ufunuo wa Yohana 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.” Mathayo 21:43 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.” Yer 1:5-10 “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Unapokuwa hujali kusimamia ulichopewa na Mungu, unaweza kukipoteza. Mungu hayuko tayari kukuacha na huduma isiyomletea matunda. Mpango wa Mungu kuhusu maisha yako hauanzii unapomjua Mungu au unapookoka bali unaanzia kabla ya kuumbwa kwako tumboni mwa mama yako. Jiulize kwa nini uko hivyo ulivyo. Kuna huduma unayotakiwa kufanya ndiyo maana umepewa akili hiyo, uwezo huo, tabia hiyo, umbile hilo, rangi hiyo nk. Usitafute maisha ambayo sio ya kwako wala usipende kuwa na mwonekano bandia. Mpe Mungu raha kwa kutomkosoa alivyokuumba. 3. Unakosa ulinzi na usalama Matendo ya Mitume 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” Najua wengi tunaposoma hii habari tunaona tu kwamba kama hujaokoka usithubutu kukemea mapepo. Tunatakiwa kuenda mbali zaidi ya hapo. Unaweza kuwa umeokoka lakini unapenda kumuinua Askofu au Mchungaji wako kuliko Bwana Yesu. Lazima utaaibika siku moja. Lakini pia unaweza kupenda kujiingiza kwenye huduma ambazo huna upako wake na kujikuta ukivamiwa na mapepo ambayo huna mamlaka ya kuyadhibiti. Tambua eneo lako na mamlaka yako vizuri. Ikibidi watumie wenye neema zingine ili usihatarishe maisha yako bila sababu. 4. Unashindwa kuthamini ulicho nacho Yn 21:19-22 “Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate. Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?) Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.” Ukisoma kuanzia mwanzo wa sura hii utaona Bwana Yesu akiongea na Petro kuhusu anavyotarajia amtumikie. Lakini Petro alipomuona mwanafunzi mwenzake akahisi kwamba yeye amepewa huduma kubwa kuliko ya kwake. Bwana Yesu hakupenda tabia yake ya kuuliza yasiyomhusu. Hivyo akamwambia nikitaka huyu asife mpaka nitakaporudi inakuhusu nini. Hutaweza kuthamini ulicho nacho kama unahangaika kujua mambo ya wengine. Timiza huduma yako uliyopewa na kuridhika nayo. Mungu anakujua sana kwamba huna uwezo wa kufanya hayo unayotamani akupe. Na kama anampenda mwingine kuliko wewe hayakuhusu. Zaidi sana tenda mazuri zaidi (pendeza zaidi) ili upendwe zaidi. 5. Unakuwa tegemezi na kushindwa kujiamini na kujisimamia Yos 1:6-9 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” Bwana alipokuwa anasema na Yoshua kwa ajili ya kuendeleza kazi aliyoachiwa na Musa alimwambia mara tatu kwamba AWE HODARI NA MOYO WA USHUJAA. Maana yake ni kwamba ajitume na kujitoa kisadaka ndipo atawafikisha watu wa Mungu katika nchi waliyoahidiwa na Bwana. Aliambiwa ajitahidi kutulia katika maono aliyopewa yaani asiende upande wa kuume wala wa kushoto. Kuna watu wanategemea kusaidiwa na watu badala ya kumuendea Mungu ili ainue watu kwa ajili yao. Tutumie muda mwingi zaidi KUMUOMBA MUNGU kuliko KUOMBA WATU ndipo tutashinda utegemezi. 6. Unapoteza utambulisho wako 1 Kor 10:12-16 “Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.” Mtume Paulo anasema anajitahidi kujali kipimo alichopimiwa na Mungu. Unapokuwa hujui mipaka ya shamba lako unaweza kuvamia la mwenzako na kujikuta umemlimia. Lakini pia unaweza kujisifia kazi ambazo walitaabika wengine na mwishowe ukajikuta hulipwi kitu mbinguni. Kuna watu wanapenda kusimulia kuhusu maendeleo ya makanisa yao lakini hawachangii kitu. Ipo siku kazi ya kila mtu itakuwa wazi kwa vile Mungu wetu anaona sirini. Mimi ninapohamasisha watu wachangie kazi ya Mungu kama kibinafsi sikutoa najua kabisa kwamba sitalipwa kwa huduma hiyo. Apandacho mtu ndicho atakachovuna. Jitambue ili usitafute kibali cha watu wengine. 7. Unaweza kufa kabla ya wakati wako Yer 11:9-11 “Naye Bwana akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu. Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao. Basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, walakini sitawasikiliza.” Unapofanya mambo ambayo yako nje ya wito wako unaweza kujikuta unaenda peke yako bila (escort) kusindikizwa na malaika. Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.” Unapoenda peke yako unahatarisha maisha yako kwa vile unakuwa huna ulinzi wa Mungu. Malaika hawezi kukulinda wala kukusindikiza kama unaenda mahali ambapo hukutakiwa kwenda au unafanya huduma ambayo hukutakiwa uifanye wewe. 8. Unaweza kupata mapigo 2 Mambo ya Nyakati 26:17-19 “Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini wa Bwana, mashujaa; wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia, Si haki yako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba, ila ni haki ya makuhani wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba; toka katika patakatifu; kwa kuwa umekosa; wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa Bwana, Mungu. Akaghadhibika Uzia; naye alikuwa na chetezo mkononi cha kufukizia uvumba; naye hapo alipowaghadhibikia makuhani, ukamtokea ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa Bwana karibu na madhabahu ya kufukizia.” Unapofanya huduma ambayo huna upako wake hata kama una madaraka au uongozi unaweza kupigwa na Mungu aliyetoa huduma. Mfalme Uzia alikataa ushauri wa makuhani kwamba hakupewa huduma ya kufukiza uvumba. Alipong’ang’aniza akapigwa na ukoma katika kipaji cha uso. Hata leo wapo watu wamepigwa ukoma katika huduma zao kiasi kwamba hawana kibali wala upako tena zaidi ya kuzungumzia walivyotumiwa zamani. Tambua umepewa nini na hukupewa nini. 9. Mungu anaweza kukukataa 1 Sam 13:10,11,13,14 “Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi. Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile Bwana alilokuamuru.” Samweli anaonekana kama wa mwisho katika watumishi ambao walikuwa na upako wa kinabii, kikuhani na kifalme (triple anoiting). Hata hivyo kwa vile watu waliomba kuwa na mfalme kama mataifa mengine tukaanza kuwa na wafalme ambao sio makuhani tena. Mfalme Sauli alikataliwa na Mungu pale alipojiingiza kwenye huduma ambayo hana upako wake wala agizo la ki-Mungu. Sio tu kwamba alikataliwa bali Mungu akainua mwingine anayeupendeza moyo wake ili achukue nafasi yake. Hata leo tuna watumishi wamekataliwa ila hawajui. Matokeo yake mambo hayaendi mpaka walazimishe kwa nguvu za kibinadamu. 10. Hutajua mipaka yako (hutajua kama umemaliza kazi yako) 2 Timotheo 4:7,8 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.” Kama unaishi maisha ambayo sio ya kwako hutaweza kujua vizuri mipaka yako ya huduma. Hebu jiulize kama unaamua kulima shamba bila kujua kwanza mipaka yake. Unaweza kujikuta umelima kipande cha shamba la mtu wakati la kwako mwenyewe hujalimaliza. Mtume Paulo ni kati ya watumishi ambao walijua ukubwa wa huduma zao na watakacholipwa baada ya utumishi wao. Paulo alisema MWENDO NIMEUMALIZA ingawa hakuja Tanzania kwa vile alijua eneo la huduma yake. Lakini pia alikuwa na bidii kwa vile alijua atapewa taji gani siku ile. Unadhani mwajiriwa atatumika kwa kujituma na kuwajibika kama hajui atalipwa nini mwisho wa mwezi? Hata wewe hutajitoa kisadaka mpaka utakapojua umelima kiasi gani, umebakiza kiasi gani na utatapata nini baada ya kumaliza kazi yako. MAOMBI YANGU KWAKO: Nakuombea Mungu akusaidie kutambua kipengele kinachokuhusu katika ujumbe huu na kukifanyia kazi ili uishi maisha uliyopangiwa na Mungu. Jitambue katika Jina la Yesu aliye hai. Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments