Ticker

6/recent/ticker-posts

Athari za kutokuwa na mpango katika maisha

ATHARI ZA KUTOKUWA NA MPANGO KATIKA MAISHA Tumekuwa na wakati mzuri wa kuandaa mpango kazi wetu wa mwaka. Watu wengi wanaishi ‘BORA LIENDE’. Sio mpango wa Mungu tuishi bila malengo wala mpango katika maisha. Neno la Mungu linasema nini kuhusu kuwa na mpango? 1. Mungu alifanya kikao kabla ya kuumba. Na katika kikao hicho alishirikisha mpango wake – tufanye mtu kwa mfano wetu. Mwa 1:26a “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” Mambo mangapi ya kifamilia au kijamii tunayapanga bila kushirikisha watekelezaji muhimu. Mfano, baba unaamua kujenga nyumba peke yako bila kushirikisha wazo lako kwa familia. Matokeo yake familia haikuungi mkono kwa vile hakuna ushirikishwaji wowote ingawa wazo lako ni zuri. 2.Mungu hakuumba vitu vyote kwa siku moja na hakuenda hatua nyingine bila kutathmini na kuhakikisha amefanya vizuri katika hatua ya kwanza. Unadhani Mungu alishindwa kuumba vitu vyote kwa siku moja? Alichukua siku sita ili kutufundisha kuwa na mpango. Mwa 1:17-19 “Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne.” 3. Mungu hakumuumba mwanadamu mpaka alipohakikisha mahitaji ya msingi ameyaandaa kwanza. Vitu vingapi tunakurupuka na kuvifanya kabla ya kuandaa kwanza mahitaji ya msingi? Mwa 1:31 “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.” Vitu vingi vinakufa kwa vile havikuandaliwa mazingira fanikishi. Mungu alijua Adamu hataishi kama atamuumba kabla ya mahitaji ya msingi ya maisha. Ndiyo maana akasubiri mpaka siku ya sita. ATHARI ZA KUTOKUWA NA MPANGO 1. Hutajua kama umefaulu (umepata faida) au umeshindwa (umepata hasara). Gal 6:4 “Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.” Watu wengine wanajisifu kwa kazi zao lakini hawajawahi kuzipima wala kuzifanyia tathmini. Na huwezi kupima kazi ambayo haiko kwenye mpango maalum. Mtu fulani aliyejulikana kwamba ni tajiri mkubwa hapa nchini aliwahi kufanyiwa tathmini na mwanae aliyemsomesha masuala ya uchumi, akashangaa kugundua ni mtu masikini kuliko watu wanavyojua. Watu wengi wanavyoonekana kwa nje sivyo walivyo katika uhalisia. 2. Hutaweza kuwa na vipaumbele (priorities). Utafanya chochote kinachokuja mbele yako. Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Mungu hakutuumba kama kikaragosi (puppet) bali ametupa utashi ili tufanye uchaguzi tunataka kuwa nani. Hatima ya maisha yetu iko mikononi mwetu. Tusipende kumsingizia shetani kwa kila tatizo tulilo nalo. Anachofanya shetani ni kushawishi lakini sio kulazimisha. Ndiyo maana hakuna mzinzi amewahi kujishangaa amevuliwa nguo na shetani bali anavua mwenyewe. Lazima kujua unaanza na nini na kinafuata nini. Ukikosea hapo unaweza kushindwa kabisa kwa vile baadhi ya shughuli zinategemeana. Lazima ujiulize kulingana na kiwango cha maisha yako kama unatakiwa uanze kumiliki hicho unachotaka. 3. Hutavutia mtu kukusaidia. Mit 22:29 “Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.” Ni vigumu kumsaidia mtu ambaye hana mpango unaoeleweka. Unadhani kwa nini watu wengi wanachangiwa harusi lakini katika maeneo mengine ya maisha hawapati michango? Harusi ina mpango unaoeleweka ndiyo maana inavutia kuchangia – kuna kamati, vikao, bajeti, tarehe ya mwisho (deadline) nk. Mpango unakufanya uwe na bidii katika jambo moja kiasi cha kuvutia wakuu na wafadhili katika kukusaidia. Hakuna mtu anapenda kumsaidia watu kila mara. Inavutia kumsaidia mtu mara moja kwa jambo ambalo hatakuuliza tena. Ukitaka kuthibitisha hili ninalosema, nenda kumuomba mtu chumvi kwa siku tatu mfululizo. Atakuchoka ingawa umeomba kitu kidogo sana. Niliwahi kupata ushuhuda wa bibi yetu kwamba mtu akimuomba kuchuma matunda mara ya kwanza alimruhusu. Akija mara ya pili alikuwa anampa mbegu. Wapo waliomuelewa vibaya lakini alitaka kuwaondoa watu kwenye utegemezi. 4. Utakuwa na viporo vingi vya kazi (kazi ambazo hazijaisha). Lk 14:28 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?” Wacha Mungu wengi wanadhani ukiwa mtu wa imani huna haja ya kuwa na mipango. Wanasahau kwamba imani sio hisia bali ni uhakika (assurance). Kama hujisikii uhakika moyoni hiyo sio imani ni kitu kingine ulichoanzisha mwenyewe. Pamoja na kumngoja Bwana lazima mtu afanye maandalizi fulani. Mit 16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.” Mpango unakusaidia ujue ukubwa wa shughuli (kujenga mnara), gharama inayohitajika na uwezo wako. Usanii (ujanja) hauko tu kwenye maeneo mengine ya maisha bali pia hata katika watu wa imani. Mtu anasingizia imani au vitabu vitakatifu hata pale ambapo yeye ndiye anatakiwa kuwajibika. Matokeo yake tuna miradi mingi ambayo haikamiliki au imefeli na tunataka kuanzisha mingine inayofanana nayo bila aibu yoyote. 5. Pesa zitakuishia kabla hujamaliza shughuli zako. Lk 14:29a “Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi.” Unapokuwa huna mpango, pesa zitaisha mapema sana. Si jambo geni pesa kuisha kabla ya mradi kumalizika ndiyo maana tunashauriwa tuwe na asilimia 10 ya ziada (contingency) kwa ajili ya dharura zinazoweza kujitokeza. Lakini inasikitisha zaidi kama pesa zitaisha baada tu ya kumaliza msingi badala ya kabla ya kupiga bati. Mtu ambaye hana mpango anasahau mambo mengine yanayotumia pesa zake kwa kiasi kikubwa kv kusomesha mdogo wake, kusaidia wazazi wake, kulipa kodi mbalimbali nk. Yapo majukumu mengi ya maisha yanayomaliza pesa kuliko tunavyofahamu kwa vile hatuweki kumbukumbu. Niliwahi kumwambia mke wangu tuandike kila tunachotumia kwa mwezi mzima ili tujue tunatumia shilingi ngapi kwa mwezi na matumizi makubwa yako eneo gani. Tulishangaa sana kwamba tunatumia sukari kwa kiwango kikubwa sana. Ilibidi familia tuulizane kama kuna watu wanalamba sukari. Kwetu matumizi makubwa yalikuwa sukari hatujui kwako ni nini. Pengine ni vocha au umeme nk. Na kama mtagundua haikwepeki kutumia kitu fulani kwa kiwango kikubwa basi afadhali mnunue kwa bei ya jumla. 6. Utafanya manunuzi ya kukurupuka (impulse buying). Ukiwa huna mpango utaanzishiwa mahitaji na wauzaji au marafiki zako. Anaweza kupita mmachinga na chupa za chai na kujikuta unaongeza mbili wakati zipo zingine nyumbani hazitumiki. Au rafiki yako anaweza kukukopesha kitu ambacho hakikuwa hitaji lako. Sisemi ni vibaya kuwanunuza watu. Nataka tu kukusaidia ili ufikie ndoto za familia yako. Watu wengi hawajui tofauti ya kuzunguka madukani kujua bei za vitu (window shopping) na kufanya manunuzi. Ukitaka ufanye manunuzi makini unashauriwa uende siku moja kujua tofauti za bei halafu siku nyingine uende kufanya manunuzi. Niliwahi kufanya hivyo Kariakoo Dar miaka zaidi ya 10 iliyopita. Nilishangaa kukuta kifaa kikiuzwa duka fulani kwa tofauti ya bei ya shilingi laki moja hivi. Mpango unakusaidia pia usinunue kitu ambacho hakitatumika kwa sasa. Unaweza kushangaa mtu amenunua kifaa kinachotumia umeme wakati nyumba yake haina umeme na wakati huohuo ana mahitaji mengine lukuki. 7. Kuna wakati utachekwa au kudhihakiwa. Lk 14:29,30 “watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.” Bwana Yesu anasema ukifanya vitu vinavyoishia njiani unaweza kuchekwa. Ukienda kwa mpango hakuna mtu atagundua kwamba umeishiwa kwa sababu unaenda kwa hatua zinazoeleweka. Mfano badala ya kujenga nyumba ya vyumba 6 na sebule halafu ikwame kabla ya ring beam (lenta) unaonaje kama ungechagua ramani inayokuruhusu ukamilishe vyumba vitatu? Hakuna sababu yoyote ya kujaribu kuishi maisha ya watu wengine. Ni kweli tunatakiwa kujifunza kwa wengine lakini tusijaribu kuiga kila kitu wanachofanya. Unaposikia mtaalamu akizungumzia mbegu ya mnazi jiulize udongo wa eneo lako unafaa zao gani. Chukua kanuni za kilimo na sio mbegu ya mnazi. 8. Utakuwa na vitu vingi vya thamani ambavyo havitumiki kwa faida. Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.” Tuna vitu vingi ambavyo kama tungeviuza hata kwa hasara tungepata mtaji au kitu cha kumsaidia mhitaji. Kuna siku nilishirikisha yeyote mwenye nguo ambazo hazivai azilete ili tuwasaidie wenye shida. Nilishangaa nguo nyingi zilikuwa zimewekwa tu wakati kuna watu wanafunga na kuomba ili Mungu awape nguo za kuvaa ibadani. Hutashangaa mwingine ana kanga nzuri zimetunzwa kwenye sanduku lake ingawa hazivai. Mimi mwenyewe nilishangaa kuona nina viatu vizuri sivivai na vingine vimenibana lakini niliviweka tu nyumbani. Ukiwa na mpango hutakaa na kitu kwa hasara nyumbani kwako. Pamoja na kuwa na mpango mzuri jitahidi pia kuwa na mkakati (strategy) ili usiwe msemaji sana wakati huna utekelezaji wowote. Mkakati utakusaidia kufikia malengo yako. Yak 1:23 “Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.” Yak 1:25 “Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.” Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania

Post a Comment

0 Comments